Sunday, 1 February 2015

Black Energy kuendelea kudhamini wavu


Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Wavu Tanzania (TAVA)  Augustino Agapa akisalimiana na wachezaji wa timu ya Jeshi Stars.

Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya kinywaji cha Black Energy imeahidi kuendelea kudhamini mashindano ya wavu wa ufukweni nchini ili kuuendeleza mchezo huo.
Black Energy ndio iliyodhamini mashindano ya kwanza ya taifa ya wavu wa ufukweni yaliyofanyika kwenye hoteli ya Mbalamwezi jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuchagua timu ya taifa  itakayoshiriki mashindano ya Kanda ya Tano ya Afrika.
Mashindano hayo yatafanyika jijini Dar es Salaam katika hoteli hiyo na mbali na Tanzania nchi zingine zinazotarajia kushiriki ni pamoja na Djibout, Somalia, Ethiopia. Rwanda na Burundi.
Mkurugemzi wa Black Energy nchini Amir Shanghavi alisema kuwa wataendelea kutoa fedha kwa Chama cha Mpira wa Wavu Tanzania (Tava) ili kiendelea kuandaa mashindano ya wavu wa ufukweni kwani unaweza kuifikisha mbali nchini kimataifa.
Mashindano ya Kanda ya Tano ya Afrika yatafanyika Mikocheni jijini Dar es Salaam kuanzia Februari  15 hadi 19 na Tanzania wanatarajia kuwakilishwa na timu nne zenye wachezaji nane.
Kwa mujibu wa Shanghavi, Black Energy pia ndio itadhamini maandalizi ya timu hizo za taifa za Tanzania kwa kuziweka kambini, kuzipatia vifaa na mahitaji mengine wakati wa maandalizi ya mashindano ya Kanda ya Tano.
Aidha, wachezaji wanaounda timu hizo za Tanzania zitakazowakilisha taifa ni pamoja na Zuhura Ally na Lizi John wa Jeshi Stars wanawak wakati Prisons itaundwa na Hellen Richard na Everyline Alberth.
Kwa wanaume Tanzania itawakilishwa na mabingwa wake timu ya Karafuu ya Zanzibar yenye wachezaji wawili Mohamed Ismail na Farahani Aboubakar huku washindi wa pili Jeshi Stars watakuwa na David Everist na Ford Edward.

No comments:

Post a Comment