Wednesday, 4 February 2015

Ndondi za mchujo kuanza Februari 9-14


Mabondia wakichuana katika mashindano ya taifa hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu
MASHINDANO ya mchujo ya ndondi yatafanyika kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa jijini Dar es Salaam Februari 9 Jumatatu ijayo hadi 14 ili kupata timu itakayoingia kambini kwa ajili ya kushiriki All African Games.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ndondi Tanzania (BFT) Makore Mashaga alisema kuwa, mashindano hayo maalum yatashirikisha walifanya vizuri katika mashindano ya wazi ya taifa yaliyofanyika hivi karibuni katika Uwanja wa Taifa.

Mashindano hao ya Mataifa ya Afrika yatafanyika kuanzia Septemba 4-19 Brazzaville, Congo na Tanzania ni miongoni mwa nchi shiriki.

Naye mwenyekiti wa mashindano Anthony Mwangonda alisema kuwa, maandalizi ya ngumi hizo za mchujo yanaendelea vizuri na zitatumika kuwapata mabondia 15 bora watakaounda timu ya taifa.

Alisema malengo yao mwaka huu ni kuhakikisha wanapata mabondia bora watakaofanya vizuri katika mashindano hayo ya Afrika kama ilivyokuwa zamani Tanzania ilipotamba katika ndondi za ridhaa.

Mabondia kama akina Willy Isangura, Makore Isangura, Lucas Msomba, Nassoro Michael, Emmanuel Mlundwa, Rashid Matumla, Haji Ally Matumla, Michael Yomba yomba, Hassan Matumla na wengineo waltamba katika mashindano mbalimbali ya kimataifa yakiwemo yale ya Jumuiya ya Madola.

No comments:

Post a Comment