Saturday, 7 February 2015

Yanga kulipa kisasi kwa Mtibwa Sugar? *Mchezo wa kwanza ilipokea kibano cha 2-0
Kikosi cha Yanga ambacho Jumapili kitacheza na Mtibwa Sugar.
Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Yanga ya jijini Dar es Salaam kesho Jumapili itakuwa na kibarua kigumu wakati itakapoikaribisha Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.
Timu hiyo yenye maskani yake mitaa ya Twiga na Jangwani ina kibarua cha kulipa kisasi baada ya kufungwa 2-0 na Mtibwa Sugar katika mchezo wa duru la kwanza uliochezwa kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Yanga ambayo iliengua kileleni Azam FC baada ya kuifunga Coastal Union ya Tanga kwa bao 1-0 kwenye uwanja wa Mkwakwani, ililiomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kusogezewa mbele mchezo huo ili ijiandae kwa mchezo wa kimataifa dhidi ya BDF XI ya Botswana.
Yanga inawakilisha taifa katika mashindano ya Kombe la Shirikisho la Afrika wakati Mtibwa Sugar ambao wenyewe wanacheza leo ugenini dhidi ya Polisi Morogoro, watashiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika.
Vijana hao wa Jangwani Jumapili iliyopita walitoka suluhu na timu iliyopanda daraja ya Ndanda FC ya Mtwara kwenye Uwanja wa Taifa kabla ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union mjini Tanga.
Mechi za leo Jumamosi Februari 07, 2015 ni Ndanda FC itaikaribisha Stand United ya Shinyanga katika mchezo utakaofanyika kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Mgambo JKT kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Mechi zingine leo ni Tanzania Prisons ambao wanashikilia mkia watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting huku JKT Ruvu wataikaribisha Mbeya City kwenye uwanja wa Azam Complex na Coastal na Simba mjini Tanga.


Msimamo kabla ya mechi za Jumamosi:

               Timu       MP  W    D    L    GF   GA   +/-  Pts 
     1         Young      12  6    4    2    13   7    6    22  
     2         Azam       11  6    3    2    15   8    7    21  
     3         Mtibwa     11  4    6    1    13   7    6    18  
     4         Polisi M.  13  4    6    3    10   9    1    18  
     5         JKT Ruvu   13  5    3    5    13   13   0    18  
     6         Shooting   13  5    3    5    9    10  -1    18  
     7         Coastal    13  4    5    4    10   9    1    17  
     8         Simba SC   12  3    7    2    13   11   2    16  
     9         Kagera     13  3    6    4    10   11   -1   15  
     10        Mbeya City 12  4    3    5    8    10   -2   15  
     11        Mgambo JKT 11  4    2    5    6    10   -4   14  
     12        Ndanda     13  4    2    7    12   17   -5   14  
     13        Stand      13  2    5    6    8    16   -8   11  
     14        Prisons    12   1    7   4    9    11   -2   10  

No comments:

Post a Comment