Friday, 6 February 2015

Caf yaifungia Morocco









MALABA, Guinea ya Ikweta
MOROCCO imepigwa marufuku kushiriki mashindano mawili yajayo ya Mataifa ya Afrika baada ya nchi hiyo kushindwa kuandaa fanali za mwaka huu za mashindano hayo.
Pia shirikisho la soka la nchi hiyo nalo limepigwa faini ya pauni 650,000 na kutakiwa kulipa euro Milioni 8 sawa na pauni Milioni 5.9 kutokana na kusababisha hasara.
Morocco ilithibitisha kuandaa fainali za mwaka huu za Kombe la Mataifa ya Afrika, lakini baadae ilikataa kwa madai ya kuogopa kusambaa kwa ugonjwa hatari wa ebola barani Afrika.
Nchi hiyo iliomba fainali hizo kusogezwa mbele hadi mwaka 2016, lakini Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) lilipinga ombi hilo.
Guinea ya Ikweta ilitangazwa kuchukua nafasi ya Morocco kuandaa fainali hizo za 16, wakati Morocco iliyofuzu kama mwenyeji, iliondolewa kabisa kushiriki katika fainali hizo.
Caf pia imewapiga faini wenye Guinea ya Ikweta dola za Marekani 100,000 kutokana na vurugu za mashabiki katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Ghana, ambao wenyeji walipokea kichapo cha bao 3-1.
Rais wa Shirikisho la Soka la Tunisia Wadie Jary naye pia amekumbana na kibano cha Caf baada ya kufungiwa kujishughulisha na shughuli zozote za soka baada ya chama chake kushindwa kuomba radhi baada ya kuituhumu Caf kuium timu yao.
Tunisia ilitoa tuhuma hizo baada ya kufungwa katika robo fainali na wapinzani wao Guinea ya Ikweta katika mazingira ya kutatanisha.
Fainali za Mataifa ya Afrika za mwaka huu zinatarajia kukamilika Jumapili, wakati Ghana watakapokwaana na Ivory Coast katika mchez wa fainali utakaofanyika Bata.

No comments:

Post a Comment