Sunday 8 February 2015

Yanga yalipa kisasi kwa Mtibwa




Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Yanga ya Dar es Salaam Jumapili iliutumia vizuri uwanja wake wa nyumbani baada ya kuichapa Mtibwa Sugar kwa bao 2-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa.

Ushindi huo wa Yanga (pichani) ni kulipa kisasi baada ya vigogo hao wa soka kupokea kipigo cha bao 2-0 katika mchezo wa kwanza wa ufunguzi wa ligi hiyo kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Shujaa wa Yanga alikuwa Mrisho Ngasa aliyefunga mabao yote mawili baada ya kuingia uwanjani akitokea benchi.

Kwa ushindi huo, Yanga imefikisha jumla ya pointi 25 ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 22 na hivyo kuifanya Yanga kujitanua kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 14.

Katika mchezo wa awali kwenye uwanja wa Jamhuri, mabao ya Mtibwa Sugar yaliwekwa kimiani na Ame Ally na Mussa Hassan Mgosi.

Yanga nusura ipate bao baada ya mshambuliaji wake Amis Tambwe kushindwa kufunga licha ya kuwa katika nafasi nzuri katika dakika ya tatu akipokea pasi ya Andrey Coutinho.

Mtibwa Sugar ilifanya mabadiliko katika dakika ya 28 wakati kocha wake Mecky Maxime alipowatoa Ibrahim Jeba na nafasi yake kuchukuliwa na Ibrahimu Mohamed aliyeumia.

No comments:

Post a Comment