Thursday, 5 February 2015

Yanga yaiengua Azam FC kileleni

Kikosi cha Wana Jangwani, Yanga katika picha ya pamoja.
Mwandishi Wetu, Tanga
BAO pekee lililofungwa na nahodha wa Yanga Nadir Haroub 'Cannavaro' dhidi ya Wagosi Coastal Union ya Tanga limeiwesesha Yanga kushika usukani wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mchezo huo ulipigwa jana kwenye uwanja wa Mkwakwani Mjini hapa na kushuhudiwa na watazamaji kibao.

Yanga walipata ushindi huo katika mchezo huo wa kiporo uliojaa ufundi na ubabe wa hapa na pale kutoka kwa wachezaji na mashabiki wa timu hizo.

Mkongwe Cannavaro amekuwa mchezaji muhimu wa timu hiyo licha ya umri wake mkubwa kutokana na kujituma na kuifungia timu yake mabao muhimu mara nyingi inapokwama kupata mabao.

Bao hilo pekee katika mchezo huo lililoifanya Yanga kuiengua Azam FC kileleni, lilifungwa na Cannavaro katika dakika ya 11 kwa kichwa akiunganisha mpira uliorushwa kama kona na `kiraka Mbuyi Twitte.

Kwa ushindi huo mwembamba lakini muhimu, Yanga imefikisha jumla ya pointi 22 na kuipiku mabingwa watetezi Azam FC wenye pointi 21 ambao hata hivyo bado wana michezo michache ukilinganisha na Yanga, ambao wamekamilisha mechi zao za duru la kwanza.

Coastal Union Jumamosi hii wana mtihani mwingine mgumu wakati watakapocheza na Simba katika mchezo mwingine wa ligi hiyo unaotarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua.

Ligi hiyo itaendelea tena wikiendi hii kw amichezo kadhaa huku pambano la Yanga na Mtibwa Sugar likiwa limeahirishwa ili kutoa nafasi kwa wawakilishi wa Kombe la Shirikisho kujiandaa vema kabla ya kuvaana na BDF XI ya Botswana wiki ijayo kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment