Saturday 28 February 2015

Azam FC yaendelea kuwa nyanya kimataifa



*Yanga waliosonga mbele warejea Jumapili usiku

*KMKM, Polisi Zanzibar nao waendelea kusindikiza


Na Mwandishi Wetu
AZAM FC imeendelea kushindwa kuonesha makali yake katika mashindano ya kimataifa baada ya kutolewa katika Ligi ya Mabingwa wa Afrika kufuatia kichapo cha bao 3-0 kutoka kwa El Merreikh ya Sudan na hivyo kutolewa kwa jumla a mabao 3-2.
Wawakilishi hao wa Tanzania walienda Sudan wakiwa na faida ya bao 2-0 waliyoyapata katika mchezo wao wa awali uliofanyika kwenye uwanja wao wa Chamazi huko Mbagala wiki mbili zilizopita, hivyo walikuwa wakihitaji sare ya aina yoyote au hata kufungwa 1-0 ili waweze kusonga mbele.
Katika mchezo huo,  El Merreikh pia walikosa penati baada ya mpigaji kupaisha mpira.
Hii ni mara ya pili kwa Azam kuaga michuano katika raundi ya mapema baada ya mwaka jana pia kutolewa na timu ya Ferroviaro de Beira ya Msumbiji katika Kombe la Shirikisho la Afrika.
Azam imetoka ikiwa ni saa chache baada ya KMKM ya Zanzibar nayo kutolewa licha ya kupata ushindi kiduchu wa bao 1-0 dhidi ya dhidi ya El Hilal ya Sudan, na kutolewa mashindanoni kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya kufungwa 2-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Sudani wiki mbili zilizopita.
Polisi Zanzibar ambayo inashiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho nayo leo ni sawa kama inakamilisha ratiba tu ya kutoka baada ya kufungwa 5-0 katika mchezo wa kwanza na Mounana ya Gabon. Timu hizo leo zinacheza kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar.
Polisi kama inahitaji kusonga mbele katika hatua inayofuata, inatakiwa angalau iibuke na ushindi wa bao 6-0, kitu ambacho hakiwezekani licha ya usemi wa lolote linawezekana katika soka.
Wakati mabingwa wa Tanzania Bara Azam FC wakitolewa, washindi wa pili wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita Yanga wanarejea Jumapili usiku baada ya kusonga mbele katika Kombe la shirikisho licha ya kufungwa 2-1 na BDF ya Zimbabwe.
Yanga sasa watacheza na Platnum ya Zimbabwe kati ya Machi 13-15, baada ya Wazimbabwe hao kuwafungisha virago Sofapaka ya Kenya kwa jumla ya bao 4-2.
Timu hiyo ya Zimbabwe katika mchezo wa awali ilishinda 2-1 kabla ya kuibuka na ushindi mwingine kama huo katika mchezo wa marudiano leo Jumamosi.

No comments:

Post a Comment