Wednesday 18 February 2015

Burkina Faso wamwania Keshi




Stephen Keshi.
LAGOS, Nigeria
KOCHA wazamani wa timu ya taifa ya Nigeria `Super Eagles Stephen Keshi yumo katika orodha ya makocha watatu wanaowaniwa na Burkina Faso kutaka kuifundisha timu ya nchi hiyo.
Shirikisho la Soka la Burkina Faso (FBF) pia katika orodha hiyo linafikiria kumuajiri kocha wazamani wa Ghana Milovan Rajevac na kocha wazamani wa Gabon na Niger Gernot Rohr.
"Mjerumani Rohr, Mserbia Rajevac na Mnigeria Keshi wamechaguliwa na kamisheni kuwania nafasi hiyo ya kuifundisha timu yetu ya taifa, imesema taarifa ya FBF.
"FBF imepanga kumtangaza mtu atakayechukua nafasi hiyo ndani ya wiki tatu zijazo."
Burkina Faso wanamtafuta mbadala wa kocha Mbelgiji Paul Put, aliyeachia ngazi baada ya timu hiyo kufanya vibaya katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika huko Guinea ya Ikweta.
Timu hiyo iliyoshika nafasi ya pili katika fainali za Afrika zilizofanyika Afrika Kusini mwaka 2013, ilitolewa katika hatua ya makundi katika fainali za mwaka huu, ambazo Ivory Coast ndio ilitwaa ubingwa.
Kwa sasa Keshi hana timu, baada ya kushindwa kukubaliana mkataba mpya na Nigeria kufuatia timu hiyo kushinda kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika mwaka huu.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 53 ana matumaini mafanikio yake ya nyuma na Nigeria, kwa kutwaa taji la Afrika mwaka 2013 na kufikia raundi ya pili ya Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil, kutamsaidia kupata kibarua hicho.
Rajevac aliifikisha Ghana katika fainali ya mwaka 2010 ya Mataifa ya Afrika na nane bora ya Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini.
Rohr aliipeleka Gabon katika robo fainali ya Mataifa ya Afrika mwaka 2012 fainali hizo zilipofanyikia katika ardhi ya nyumbani na aliweza kuiongoza Nigera mwaka 2013 katika mashindano hayo, lakini alishindwa kuivusha kutoka katika hatua ya makundi.

No comments:

Post a Comment