Tuesday, 24 February 2015

Azam, Yanga waenda Sudan, Botswana

Kikosi cha Azam FC.
Na Mwandishi Wetu
WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika, Azam FC na Yanga Africans wanaondoka leo na kesho kwenda ugenini kucheza mechi za marudiano.
Azam FC wanatarajia kuondoka leo Jumanne kwenda Sudan kucheza na El-Merreikh wikiendi hii mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa wa Afrika.
Katika mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye uwanja wa Azam complex Chamazi Mbagala, wenyeji waliibuka na ushindi mnono wa mabao 2-0 na hiyo kuhitaji sare au ushindi wa aina yoyote ili kusonga mbele.
Msemaji wa Azam, Jaffar Idd Maganga alisea kuwa timu yao inaondoka huku ikiwa na matumaini kibao ya kufanya vizuri katika mchezo huo na kusonga mbele hatua inayofuata.
Hii ni mara ya kwanza kwa mabingwa hawa wa Tanzania kushiriki michuano ya ligi ya Mabingwa barani Afrika kwani mara mbili walishawi kucheza Kombe la Washindi baada ya kumaliza wa pili katika Ligi Kuu Tanzania Bara nyuma ya Yanga.
Wawakilishi wengine wa Tanzania, Yanga wenyewe wanatarajia kuondoka nchini kesho kwenda Botswana kurudiana na Wajeshi BDF katika mchezo wa Shirikisho utakaofanyika wikiendi hii.
Yanga nao wanahitaji sare ya aina yoyote au ushindi ili kusonga baada ya kushinda 2-0 katika mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment