Tuesday 24 April 2018

Uchukuzi, Tanesco Soka Zakaribia Nusu Fainali Mei Mosi

Wachezaji wa timu ya wanawake ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kulia wakiongozwa na Neema Mbuja wakiwavuta wenzao wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) leo kwenye michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika Uwanja wa Samora. Tanesco walishinda kwa mivuto 2-0. (Picha na Bahati Mollel wa TAA).

 Na Bahati Mollel-TAA, Iringa
TIMU za soka za Uchukuzi na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) zilizopo kundi ‘A’ na ‘B’ zinakaribia kutinga nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mei Mosi baada ya leo kushinda michezo ya iliyofanyika kwenye uwanja wa Samora, ambapo kila mmoja zinaongoza kundi lake kwa kujikusanyia pointi sita.

Uchukuzi inafuatiwa na mabingwa watetezi Geita Gold Mine (GGM) wenye pointi mbili, NAO na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro yenye pointi moja kila mmoja; wakati Tanesco inafuatiwa na Tumbaku nayo inapointi sita lakini imezidiwa magoli ya kufunga, huku RAS Iringa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wakiwa hawana pointi.
Wachezaji wa michezo mbalimbali wa Klabu ya Uchukuzi wakishingilia mara baada ya mchezo wa soka wa michuano ya Kombe la Mei Mosi dhidi ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu (NAO) kumalizika kwa ushindi wa magoli 3-1 baada ya timu yao kushinda kwenye Uwanja wa Samora mkoani Iringa. (Picha na Bahati Mollel wa TAA).  
Katika mechi hizo za jana Uchukuzi waliwafunga Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu (NAO) kwa magoli 3-1. Nao ndio walikuwa wa kwanza kupachika bao katika dakika ya 45 kupitia kwa Peter Dihoko aliyeunganisha kona ya George Mlelwa.

Uchukuzi walisawazisha katika dakika ya 60 kupitia wa Kado Nyoni, huku bao la pili lilifungwa na Omary Kitambo dakika ya 63 na bao la tatu dakika ya 68 lililofungwa na Issack Ibrahim.

 Mfungaji Ester Turuka (GA-orange katikati) wa RAS Iringa akijaribu kuwania mpira na Cecy Kanza (WD) Tanesco katika mchezo wa michuano ya Mei Mosi uliofanyika leo kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki Iringa (RUCU). RAS Iringa walishinda kwa magoli 27-14 (Picha na Bahati Mollel wa TAA).

Nao Tanesco waliwachapa RAS Iringa kwa magoli 4-0, ambapo matatu yaliyofungwa na Kurwa Mangara katika dakika ya 19, 34 na 59 huku Salehe Bakari alifunga bao la nne dakika ya 66.

Katika mchezo wa netiboli timu ya RAS Iringa iliwafunga Tanesco kwa magoli 27-14. 

Washindi walikwenda mapumziko wakiwa mbele kwa magoli 9-7. Nayo Ikulu walipewa ushindi wa mezani wa magoki 40 na pointi mbili baada ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kushindwa kufika uwanjani Chuo Kikuu cha Katoliki (RUCU) kwa kuwa na majeruhi wengi waliotokana na kuvuta kamba.  

  Daktari wa timu ya Uchukuzi, Hawa Senkoro (kushoto) akimchua misuli mchezaji wake Kassim Sabu aliyebanwa na misuli katika mchezo wa soka wa michuano ya Kombe la Mei Mosi dhidi ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu (NAO) uliofanyika leo kwenye uwanja wa Samora, ambapo Uchukuzi walishinda kwa magoli 3-1. (Picha na Bahati Mollel wa TAA).

Katika mchezo wa kuvuta kamba kwa wanawake timu ya Uchukuzi ilivutwa na RAS Iringa 1-0 baada ya mvuto wa awali kutoka sare;  huku kwa upande wa wanaume wa Uchukuzi waliwavuta Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu (NAO) kwa mivuto 2-0.

Michezo mingine ya kamba wanawake walivutwa na MUHAS mivuto 2-0; nayo NAO waliwavuta Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mvuto 1-0 kwa upande wa wanaume.

 Mlinzi Jacky Sanga (mwenye mpira) wa Tanesco akitafuta wa kumrushia katika mchezo wa michuano ya Kombe la Mei Mosi kwa mchezo wa netiboli dhidi ya RAS Iringa uliofanyika leo kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki Iringa (RUCU). (Picha na Bahati Mollel wa TAA).

Michuano hiyo inaendelea kesho kwa upande wa netiboli wakati timu ya Uchukuzi itacheza na RAS Iringa Uwanja wa RUCU; huku katika soka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wataumana na Tumbaku ya Morogoro, na GGM watacheza na Uchukuzi kwenye Uwanja wa Samora; wakati katika kamba RAS Iringa kuumana na Tanesco kwa wanawake.
Beki George Mlelwa wa timu ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu (NAO) akipiga mpira mbele ya Andrew Kunambi (mwenye jezi ya njano mbele) wa Uchukuzi katika mchezo wa michuano ya Mei Mosi uliofanyika leo kwenye uwanja wa Samora, ambapo Uchukuzi walishinda kwa magoli 3-1. (Picha na Bahati Mollel wa TAA).


No comments:

Post a Comment