Sunday 8 April 2018

Mabondia Wote wa Tanzania Wadundwa Madola

Mabondia wa timu ya Tanzania walioshiriki Michezo ya 21 ya Jumuiya ya Madola wakiwa na kocha wao, Moses Oyombi  (katikati mbele) wakati wa mazoezi Kibaha, Pwani kabla ya kwenda Gold Coast kwa michezo hiyo, Mabondia wote wamepigwana kutolewa.

Na Mwandishi Wetu
MABONDIA wa Tanzania wote wametolewa katika Michezo ya 21 ya Jumuiya ya Madola inayoendelea Gold Coast, Australia baada ya kudundwa.

Ezra Mwanjwango naKassim Mbundwike walipoteza mapambano yao katika uzito wa bantamweight na welterweight katika ukumbi wa Oxenford.  Mabondia hao walikuwa wakicheza katika hatua ya 16 bora ili kufuzu kwa robo fainali.

Mwanjwango alipoteza pambano lake hilo lilichezeshwa na mwamuzi wa Italia Maria Rizzardo kwa majaji 5-0 dhidi ya bondia Mzambia Everisto Mulengain.

Kama hilo halitoshi, bondia mwingine wa Tanzania, Mbundwike alipoteza pambano lake dhidi ya Manoj Kumar wa India kwa pointi 5-0 na kuhitimisha mbio za Tanzania kusaka medali kwa upande wa mchezo huo.

Ijumaa mabondia wengine wa Tanzania, nahodha wa timu ya ndondi, Selemani Kidunda na Haruna Mhando walipoteza mapambano yao.
Timu ya taifa ya ndondi siku ya kuagwa kwa timu ya Tanzania iliyoshiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Bondia aliyekuwa wa kwanza kupoteza pambano lake ni Mhando aliyepoteza kwa bondia wa India, Naman Tanwar katika uzito wa juu wakati Kidunda alichapwa na kwa pointi 2-3 dhidi ya Mkenya Edwin Owuor katika pambano la middle.

Sasa Tanzania matumaini yake katika medali ni katika mchezo wa riadha, kuogelea nampira wa meza.

Mwanariadha wa Tanzania Ali Khamis Gulam leo asubuhi alikimbia katika mbio za meta 100 na kumaliza katika nafasi ya nne katika kundi lake la mchujo, na hivyo naye ameungana na mabondia wa Tanzania kuiaga michezo hiyo, lakini amebakiwa na mchezo wa mbio za meta 200.

Muda bora wa Gulam ni sekunde 10:72, ambao ni wa chini ukilinganisha na rekodi ya michezo hiyo wa sekunde 9.58 unaoshiiliwa na Mjamaica Usain Bolt, ambaye sasa amestaafu mbio.

Rekodi ya Michezo ya Jumuiya ya Madola kwa mchezo huo ni sekunde 9.88 uliowekwa na Ato Boldon huko Kuala Lumpur, Malaysia mwaka 1998.

Wachezaji wa mpira wa meza wataanza kampeni zao Jumanne, wakianza na wanawake na wanaume kwa mchezo wa mchezaji mmoja mmoja.

No comments:

Post a Comment