Friday 20 April 2018

Kigwangala Kuanzisha Ngorongoro Race kesho

Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangala.
Na Mwandishi Wetu, Karatu
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangala leo atabariki mbio za 11 za Ngorongoro Race zitakazofanyika mjini hapa na kushirikisha wanariaha zaidi ya 700 kutoka ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa mbi hizo ambazo kauli mbiu yake ni `Kimbiza Jangili’ Meta Petro, usajili wa wanaotaka kushiriki kwa mbio hizo za kilometa 21, ulitarajia kukamilika leo tayari kwa mpambano utakaofanyika kesho.

Alisema Kigwangala amethibitisha kuanzisha mbio hizo na kukabidhi zawadi kwa washindi pale zitakapokamilika na washindi kujulikana.

Alisema mbio hizo zitaanzia katika lango kuu la kuingilia na kutokea katika Bonde la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), ambao ndio pia ni wadhamini wakuu wake na kumalizikia katika viwanja vya Mazingira Bora katikati ya Mji wa Karatu.

Alisema kuwa wanatarajia mbio za mwaka huu zitakuwa na ushindani wa hali ya juu, hasa ukizingatia zitashirikisha wanariadha wengi zaid ya 500 walioshiriki mwaka jana.

Nyota mbalimbali wa mbio nchini wanatarajia kushiriki mbio hizo wakiwemo washindi wa mwaka jana kwa upande wa kiume na kike, Faraja Lazaro wa JKT na Failuna Abdi wa Talent Club ya Arusha, ambao walishinda mbio hizo kwa kutumia saa 1:03.42 na 1:03.52.

Mshindi wa kwanza wa mbio hizo kwa upande wanaume na wanawake, kila mmoja ataondoka na Sh milioni 1 wakati mshindi wa pili atabeba Sh 500,00 huku watatu Sh 250,000, mshindi wan ne atapewa 100,000 na watano Sh 80,000.

Kwa mujibu wa waandaaji, mbio za mwaka huu zitakuwa na zawadi hadi kwa mshindi wa 15 huku mshiriki yeyote atakayemaliza mbio hizo katika nafasi yoyote, atapewa medali pamoja na fulana kama kumbukumbu za kushiriki mbio hizo.

Mbali na kilometa 21 pia kutakuwa na mbio za kilometa tano, ambapo kwa mara ya kwanza washindi watapewa zawadi, kwani mbio hizo ni za kujifurahisha na waandaaji wamekuwa hawatoi zawadi kwa washindi.

Mshindi wa kwanza wa kilometa tano ataondoka na kitita cha Sh 200,000  wakati mshindi wa pili ataondoka na Sh 100,000 huku mshindi watatu kwa kila upande, atasepa na Sh 50,000.

Pia, kutakuwa na mbio za watoto wadogo, ambao watachuana katika umbali wa kilometa 2.5, ambapo mshindi wa kwanza ataondoka na Sh 50,000, huku wa pili atabeba Sh 40,000 na watatu Sh 30,000.


Mbali na NCAA, wadhamini wengine ni Kampuni ya Vinywaji Baridi ya Bonite Botlers.

No comments:

Post a Comment