Monday 9 April 2018

Kocha Lwandamila Awaonya Wachezaji Yanga


Na Mwandishi Wetu
LICHA ya ushindi mnono ulioiweka katika nafasi nzuri ya kukaribia kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, kocha wa Yanga George Lwandamina, amewataka wachezaji wake kutowadharau wapinzani wao Welayta Dicha.

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, hivyo kujiweka mguu moja mbele katika harakati za kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa katika ngazi ya klabu Afrika.

Akizungumza na gazeti hili Lwandamina alisema Welayta Dicha na timu nzuri na wanapaswa kujiandaa kikamilifu ili kuweza kuwadhibi wakiwa kwao vinginevyo wanawezakujikuta katika wakati mgumu na ikiwezekaa kupoteza nafasi ya kucheza hatua ya makundi.

“Mbali na mbinu za kucheza ugenini, ambazo nimeanza kuwafundisha vijana wangu lakini kitu kingine cha muhimu nimekuwa nikiwakumbusha kwamba bado tuna kibarua kizito na ushindi tulioupata hapa nyumbani unapaswa tuulinde kwa kucheza kwa kushambulia ili tupate mabao mengine,” alisema Lwandamina.

Kocha huyo raia wa Zambia alisema kitu cha msingi ameamua kuanza nacho katika marekebisho yake kabla ya mchezo huo ni safu yake ya ulinzi, ambayo ilifanya makosa mengi ikifuatiwa na ile ya ushambuliaji ambayo nayo ilipoteza nafasi nyingi walizotengeneza.

Alisema kama wangeweza kuzitumia vizuri nafasi zote walizozipata kazi yao katika mchezo wa marudiano ingekuwa nyepesi lakini mabao mawili bado hayampi uhakika wa kusonga mbele kutokana na ubora wa wapinzani wao ambao watakuwa nyumbani Addis Ababa.

Yanga inatarajiwa kuondoka nchini mwishoni mwa wiki hii kuelekea Ethiopia ambapo ndiko utakapofanyika mpambano huo na endapo watafanikiwa kusonga mbrele watacheza hatua ya makundi ya michuano hiyo kama ilivyokua mwaka 2016 chini ya kocha Hans van der Pluijm.

No comments:

Post a Comment