Monday 9 April 2018

Wanafunzi Wawili Watanzania Wang'ara Mbio za Kusaka Tuzo za Kimataifa za DStv Eutelsat Star

Na Mwandishi Wetu
Tanzania imepata wawakilishi wawili watakaoshiriki katika msimu wa saba wa tuzo maarufu barani Afrika kwa wanafunzi wapenzi wa masomo ya Sayansi na Teknolojia ijulikanayo kama - DStv Eutelsat Star Awards. 

Wanafunzi hao Michael Ditrick wa shule ya Sekonday Ilboru – Arusha na Taher Rasheed wa Al-Madrasat Ussaifiyatul Burhaniyah ya jijini Dar es Salaam
 Michael ameshika nafasi ya kwanza katika uandishi wa insha maalum na Taher kwa mchoro maalum kuhusiana na sayansi ya Setelait ambapo wanafunzi zaidi ya 150 kutoka shule mbalimbali nchini walishiriki katika mashindano hayo ya mwaka huu. Washindi hao walipatikana kutakana na utahini uliofanywa na jopo la majaji sita.
 Kazi za washindi hao zimewasilishwa MultiChoice Africa ambapo zitapambanishwa na kazi kama hizo kutoka kwa washindi wa nchi nyingine kote barani Afrika na hatimaye kupatikana mshindi wa jumla katika kila kipengele yaani wale walioandika insha na wale walioandaa mchoro.
 Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania Maharage Chande, amesema tuzo za mwaka huu zimekuwa na ushindani mkubwa ambapo shule kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Mwanza, Dar es Salaam, Mbeya, Arusha, Dodoma, Pwani zimeshiriki. 

“Kuongezeka wa idadi ya wanafunzi wanaoshiriki katika tuzo hizi ni ishara njema na tunaamini kwa viwango walivyoonyesha, bila shaka mwaka huu tutapata ushindi mkubwa kuliko hata ule wa mwaka jana” alisema Maharage.
 Amesema tuzo hizi zinalenga kuwajengea vijana wetu ari ya kushiriki katika masomo ya sayansi na pia kuhamasisha ubunifu na ugunduzi katika tasnia ya sayansi. 
Amewataka walimu kuwahimiza wanafunzi wao kushiriki katika tuzo kama hizi za kimataifa kwani ni kipimo kizuri kwa wanafunzi wetu na pia inajenga kujiamini kwa wanafunzi wetu.
 Tuzo hizi ambazo zinahusisha uandishi wa insha maalum au kuandaa bango vyenye ujumbe kuhusiana na elimu ya anga hususan Setelait ni za wazi kwa wanafunzi wote wa shule za sekondari wenye umri kati ya miaka 14 – 19.
 Mwaka huu, washindani walitakiwa kuandika insha au kubuni bango kuhusu manufaa yaliyoletwa na uvumbuzi wa setelaiti katika maisha ya kila siku hapa ulimwenguni na ni jinsi gani setelait imekuwa kama kiungo muhimu kwa shughuli zote zinazofanyika kote duniani.
 Kama kawaida tuzo hizi zina zawadi kabambe ambapo mshindi wa Insha atapata fursa ya kuzuru kituo cha Eutelsat nchini Ufaransa na pia kwenda Guiana kushuhudia mubashara urushwaji wa setelait angani.
 Mshindi wa bango atajishindia safari ya kwenda nchini Afrika Kusini na kutembelea kituo cha anga cha nchi hiyo na pia makao makuu ya MultiChoice Africa akiwa kama mgeni maalum.  Shule zitakazotoa washindi hao zitapata zawadi ya kufungia huduma ya DStv bure.

 Wanafunzi wengine waliofanya vizuri katika mchakato huo ni pamoja na Pio Mwita wa UWATA Sekondari ya Mbeya ambaye ameshika nafasi ya pili kwenye insha na Peter Kiama wa Feza Boys ya Dar es Salaam aliyeshika nafasi ya pili kwa upande wa bango.

Mwaka jana Tanzania iliibuka mshindi wa pili kwenye insha baada ya Davids Bwana wa FEZA Boys kunyakua nafasi hiyo nyuma ya mwanafunzi Leoul Mesfin kutoka Ethiopia.

No comments:

Post a Comment