Wednesday 11 April 2018

Nane Bora Ligi ya Wanawake Kuendelea Aprili 21

Na Mwandishi Wetu
VINARA wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara, JKT Queens wanatarajia kushuka dimbani Aprili 21 kucheza na Simba Queens kwenye Uwanja wa Mbweni nje kidogo ya jijini la Dar es Salaam.

Akizungumza jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Cliford Ndimbo alisema hatua ya Nane Bora, inatarajia kuendelea Aprili 21 kwenye viwanja vinne tofauti.

“Ligi ya wanawake hatua ya Nane Bora ilisimama kupisha maandalizi ya timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) iliyokuwa kambini kujiandaa na mchezo wa kufuzu fainali za Africa kwa Wanawake, hivyo sasa itaendelea katika mzunguko wa Tano kuanzia Aprili 21,” alisema Ndimbo.

JKT Queens inaongoza ikiwa na pointi 12 baada ya kucheza michezo minne na kushinda yote, huku Simba Queens ikishika nafasi ya sita ikiwa na pointi tatu baada ya kucheza michezo minne na kufungwa mitatu.

Kigoma Sisters inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi tisa itaikaribisha Baobab ya Dodoma kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Baobab inashika nafasi ya tano ikiwa na pointi tano baada ya kucheza michezo minne, ikishinda mmoja, sare mbili na kufungwa mmoja.

Mabingwa watetezi, Mlandizi Queens watakuwa ugenini kucheza na Panama kwenye Uwanja wa Samora Iringa. Mlandizi ina pointi sita katika michezo minne iliyocheza na Panama,  inashika nafasi ya saba ikiwa na pointi mbili katika michezo minne iliyocheza.

Alliance Girls inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi saba, itakuwa ugenini kucheza na Evergreen, ambayo inaburuza mkia ikiwa na pinti moja kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment