Friday 6 April 2018

TFF Yatupa Tena Rufaa ya Michael Wambura


Na Mwandishi Wetu
KAMATI ya Rufaa ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imetupa rufaa ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa TFF, Michael Wambura kufungiwa maisha kujihusisha na shughuli za soka.

Akisoma hukumu hiyo jana Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya TFF, Ebenezer Mshana alisema kamati yake ilipitia hukumu tatu, ambazo zilikatwa kwa kamati hiyo dhidi ya TFF.

Mshana alisema baada ya kupitia hukumu zote tatu na hoja za rufaa, rufaa moja ya Edgar Chibula ilishinda na rufaa mbili ambazo ni ya Wambura na Dustan Mkundi, kamati imejiridhisha na maamuzi ya awali yaliyotolewa na Kamati ya Maadili kuwafungia maisha.

“Upande wa utetezi wa Wambura ambao ulikuwa na mawakili watatu ukiongozwa na Masumbuko Lamwai, ulileta mbele ya kamati hoja nne za kupinga mteja wao kufungiwa maisha kujihusisha na soka na upande wa TFF uliwakilishwa na wanasheria wawili ikiongozwa na Allan Kiluvya,” alisema Mshana.

“Katika barua yake ya Desemba 4, 2016 Kamati ya Maadili ya Rufaa imejiridhisha kuwa Wambura alipewa nafasi ya kujieleza kwani alitakiwa kufanya na Kamati ya Ukaguzi na ushahidi wa video uliwasilishwa mbele ya kamati hiyo,” alisema Mshana.

Katika hoja za rufaa kamati ilisikiliza pande zote mbili za rufaa na upande uliokatiwa rufaa ambao ni TFF baada ya kusikiliza pande zote mbili kamati ilijiridhisha na maamuzi ya kamati ya maadili.

Kamati ya TFF ilimfungia kujihulisisha na soka maisha Makamu wa Rais wa TFF, Michael Wambura  baada ya kumkuta na hatia katika tuhuma tatu zilizokuwa zinamkabili kwa mujibu wa Kifungu cha 73(1)(c) cha Kanuni za Maadili ya TFF toleo la 2013 kama zilivyofikishwa kwenye kamati na sekretarieti ya TFF.

Wambura alifikishwa kwenye Kamati ya Maadili na Sekretarieti ya TFF kwa makosa ya kupokea/kuchukua fedha za TFF kwa malipo yasiyo halali na kughushi barua ikiwa ni kinyume na kifungu cha 73(1) cha Kanuni za Maadili za TFF Toleo la 2013.”

Kufanya vitendo vinavyoshusha hadhi ya Shirikisho ikiwa ni kinyume na ibara ya 50(1) ya Katiba ya TFF (kama ilivyorekebishwa 2015).

Kamati ya Rufaa ya Maadili imeiagiza TFF kulifikisha suala la Wambura na Danstun Mkundi kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zingine za kisheria na imebariki kifungo cha maisha cha kutojihusisha na soka maisha.

Kwa upande wa wakili wa Wambura, Muga alisema mteja wake hajaridhishwa na hukumu hiyo, hivyo atakata rufaa katika ngazi nyingine.

No comments:

Post a Comment