Monday 9 April 2018

Ronaldo afunga, Real ikitoka sare na Atletico

MADRID, Hispania
 MSHAMBULIAJI wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo ameifungia timu yake katika sare ya bao 1-1 dhidi ya Atletico Madrid katika mchezo wa Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’ uliochezwa juzi kwenye uwanja wa nyumbani, akifunga katika mchezo wa 10 mfululizo.

Lakini Antoine Griezmann alisawazisha baadaye na kuendelea kubaki katika nafasi ya pili na kuwaacha Madrid inayowafuata kwa tofauti ya pointi nne.

Sare hiyo inaendelea kuwapa nafasi vinara wa La Liga Barcelona ya kushinda taji baada ya kumuacha Atletico kwa tofauti ya pointi 11, huku Madrid ikishuka hadi nafasi ya nne na Valencia ikipanda juu baada ya kushinda 1-0 dhidi ya Espanyola.

Barcelona inaongoza kwa pointi 79 baada ya kuichapa Leganes 3-1 Jumamosi, ikifuatiwa na Atletico yenye pointi 68, Valencia 65 na Real 64 baada ya kila mmoja kucheza michezo 31. Barca inaweza kuchukua taji kama itashinda michezo minne kati ya saba ijayo.

“Siwezi kuwa na furaha kwa sare kwa sababu tulihitaji ushindi,” alisema Kocha wa Atletico, Diego Simeone.

“Walianza kucheza vizuri, tulipambana kucheza kwa umoja lakini kipindi cha pili tulishambulia zaidi na kutengeneza nafasi, walitufunga na tukafanikiwa kurudisha haraka, tunaondoka tukijivunia kwa kidogo tulichopata,” alisema.

Kocha wa Madrid, Zinedine Zidane alisema “Nina furaha na jinsi tulivyocheza ingawa tulistahili zaidi, ni aibu tulishindwa kushinda kwa sababu tulitengeneza nafasi nyingi lakini pia, tungepoteza mchezo.”

No comments:

Post a Comment