Monday 16 April 2018

Ni Mwaka wa Simba 2018 Yaendelea Kutoa Vichapo


Na Mwandishi Wetu
JOHN Bocco na Emmanuel Okwi walizidi kuipeleka Simba jirani na taji la Ligi Kuu Bara baada ya kuiwezesha timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania bara uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Ushindi huo unaifanya Simba izidi kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, kwani sasa inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 58 juu ya mabingwa watetezi Yanga walio na pointi 47 na mechi mbili kibindoni.

Mabao ya Simba yalifungwa katika kila kipindi kwenye mechi hiyo hiyo ambayo vinara hao walitawala katika vipindi vyote.

Prisons ilionekana kuibana Simba katika dakika za mwanzo kabla ya kusalimu amri na kuruhusu bao la Bocco dakika ya 35 kabla ya kujikuta wakicheza mchezo wa kujilinda zaidi katika kipindi cha pili.
Bocco alifunga bao hilo la kuongoza kwa kuuwahi kwa kichwa mpira wa krosi wa Erasto Nyoni uliogonga mwamba kabla ya kuujaza wavuni.

Okwi aliifungia Simba bao la pili katika dakika ya 80 na kuendelea kukifukuzia kiatu cha dhahabu kwa kufikisha mabao 18 kwenye ligi.

Penalti ya Okwi ilitolewa na mwamuzi Shomari Lawi wa Kigoma baada ya Jumanne Elifadhili kumfanyia madhambi Bocco akiwa kwenye eneo la hatari, Elifadhili alioneshwa kadi nyekundu.

Katika mechi hiyo Simba ilikosa mabao mengi hasa kupitia kwa mchezaji wake Shizza Kichuya aliyekosa mabao dakika ya kwanza, 50, 62 na 70.

Mechi nyingine za ligi hiyo ni Ndanda ikiwa nyumbani Nangwanda Sijaona imeshindwa kutamba kwa kukubali ‘kupapaswa’ na Ruvu Shootinga kwa mabao 3-1, huku Kagera Sugar ikishinda 2-1 dhidi ya ndugu zao Mtibwa Sugar kwenye uwanja wake wa nyumbani Kaitaba.

No comments:

Post a Comment