Wednesday 11 April 2018

Simba Kibaruani Ikiikaribisha Mbeya City Taifa


Na Mwandishi Wetu
WEKUNDU wa Msimbazi na Vinara wa Ligi Kuu Bara Simba, kesho inashuka dimbani kukipiga na Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.

Simba, inashuka dimbani ikihitaji pointi tatu muhimu ili kujisogeza zaidi kwenye mbio za kuwania ubingwa wa ligi hiyo, wakati Mbeya City ikihitaji nafasi ya saba.

Kuelekea mchezo huo Wekundu wa Msimbazi watakuwa na faida ya urejeo wa wachezaji wao watatu, Juuko Murushid, James Kotei na Erasto Nyoni, ambao walikua wanatumikia adhabu yao ya kadi tatu za njano kwa kila mmoja.

Tayari wachezaji hao wamemaliza adhabu hiyo na leo watakuwa sehemu ya kikosi cha Simba.

Aidha, Mbeya City inawakosa wachezaji wake muhimu ambao ni,John Kabanda na Hassan Mwasapili, ambao wana matatizo tofauti.

Kocha wa timu hiyo, Ramadhani Nswanzurimo alisema pamoja na kuwakosa nyota hawa bado ana matumaini ya kuondoka na pointi tatu kwenye mchezo huo, kwani tayari ameandaa mbadala wa wachezaji hao.

Alitaja kuwa wachezaji, Haruna Shamte na Rajab Isihaka watachukua nafasi hizo kwa ajili ya kuhakikisha wanaidondosha Simba katika mchezo huo.

Mchezo huo utakuwa wa raundi ya 23 kwa Simba, lakini 24 kwa Mbeya City,  ambaye mpaka sasa imefikisha pointi 26 na wapinzani wao wakiwa kileleni kwa alama 52 kwenye msimamo wa ligi.

Michezo mingine itakayopigwa leo ni Mtibwa Sugar ambao wamekuwa na mwenendo mzuri hivi karibuni itacheza na Ndanda katika dimba la Manungu Mkoani Morogoro, wakati Azam FC itakuwa wageni wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mabatini Pwani.

No comments:

Post a Comment