Monday 30 April 2018

Hans Pope Aungwanishwa Kesi ya Aveva


Na Mwandishi Wetu
MAHAKAMA ya  Hakimu Mkazi Kisutu, imeamuru Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Klabu ya Simba, Zacharia Hans Pope na mwenzake wakamatwe na kufikishwa mahakamani hapo ili waunganishwe katika kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili, Rais wa Klabu  hiyo, Evans Aveva na makamu wake, Godfrey Nyange 'Kaburu'.

Pamoja na Hanspope mahakama hiyo imeamuru  Franklin Lauwo naye akamatwe afikishwe mahakamani hapo.

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alitoa amri hiyo jana mara baada ya Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai kubadili hati ya mashitaka na kuongeza washitakiwa hao.

Wakili Swai alidai kuwa washitakiwa hao wawili wametafutwa na taasisi hiyo tangu mwezi wa tatu bila mafanikio.

Hivyo, aliomba hati ya kuwakamata washitakiwa hao ambao hawakuwepo mahakamani wakati hati ya mashitaka inabadilishwa na kuwaunganisha kuwa miongoni mwa washitakiwa wa utakatishaji fedha na kughushi.

Inadaiwa Machi 15, mwaka jana, jijini Dar es Salaam, washitakiwa Aveva na Nyange wote kwa pamoja walighushi fomu ya kuhamisha fedha kuonesha kwamba Klabu ya Simba inalipa deni la dola za Marekani 300,000 kwa  Aveva, kitu ambacho si kweli.

Katika shitaka la pili linalomkabili Aveva, inadaiwa Machi 15, mwaka jana maeneo ya Benki ya CRDB tawi la Azikiwe wilayani Ilala, Dar es Salaam, alitoa nyaraka hiyo ya uongo kwa benki hiyo kuonesha kuwa klabu hiyo inalipa dola za Marekani 300,000 kwa Aveva.

Pia inadaiwa  tarehe tofauti tofauti kati ya Machi 15 na Juni 29, mwaka jana, ndani ya mkoa huo, washitakiwa walikula njama kutakatisha fedha dola za Marekani 300,000 huku wakijua kwamba fedha hizo ni zao la uhalifu ambalo ni kughushi.

Machi 15 mwaka jana, katika Benki ya Barclays Mikocheni wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Aveva alijipatia dola za Marekani 300,000 wakati akijua kuwa alipata fedha hizo kutokana na nyaraka za kughushi.

Katika mashitaka ya tano yanayomkabili Nyange, ilidaiwa Machi 15, mwaka jana katika tawi la Barclays tawi la Mikocheni, alimsaidia Aveva kupata fedha kutoka katika benki hiyo, huku akijua kwamba ni zao la uhalifu, ambalo ni kutokana na kughushi fomu ya kuhamishia fedha.

No comments:

Post a Comment