Wednesday 11 April 2018

Yanga Sports Yataka Mashabiki kuwa Watulivu


Na Mwandishi Wetu
KLABU ya Yanga imewataka mashabiki wake kuwa watulivu kufuatia kuondoka kwa Kocha wao George Lwandamina (pichani) baada ya kurudi katika timu yake ya zamani ya Zesco United ya Zambia.

Mwenyekiti wa Kamati ya mashindano Yanga Hussein Nyika alithibitisha jana kuondoka kwa Lwandamina akisema kuwa wataweka wazi taarifa kamili ya sababu ya kutimka kwake baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji kilichotarajiwa kukaa jana jioni.

Kwa mujibu wa gazeti la Lusaka Times, Lwandamina amejiunga na Zesco United baada ya kuondoka katika klabu hiyo mwaka mmoja na nusu uliopita.

 “Ni kweli Kocha ameondoka tunaomba mashabiki wawe watulivu, tunatarajia kukaa kikao cha Kamati ya utendaji jioni baada ya mechi ya Singida United (jana) kisha tutatoa taarifa ya klabu,”alisema.

Mkataba wa kocha huyo Mzambia ulitarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu kwa maana ya mwezi ujao lakini klabu ya Zesco United iliweka taarifa juzi za kumtangaza Kocha huyo kujiunga nao.

Kitendo cha kuondoka kwake ghafla huku timu hiyo ikiwa na mechi muhimu za ligi na kimataifa, kimewaacha mashabiki katika mshangao.

Nyika alisema watazungumza na Lwandamina kujua tatizo lililomkimbiza ghafla akitoa matumaini kwa mashabiki kuwa kocha huyo atarudi.

Lwandamina aliinoa Zesco kati ya mwaka 2014 na 2017  na kujiunga na  Yanga msimu uliopita ambapo aliipa taji la ligi.  Ni mmoja kati ya makocha wenye majina makubwa nchini Zambia kutokana na kujiwekea wasifu mkubwa katika maisha yake ya ukocha nchini humo.

Aliwahi kuwa Kocha wa timu kubwa ya taifa ya Zambia na timu za vijana kwa miaka tofauti.

No comments:

Post a Comment