Monday 23 April 2018

Uchukuzi Mabingwa Mbio za Baiskeli Mei Mosi 2018


 Bingwa wa mchezo wa baiskeli kwa wanaume, Chaptele Muhumba (aliyenyoosha mkono) wa Uchukuzi akiwa na wasindikizaji wake mara baada ya kumaliza mbio za kilometa 20 zilizoanzia eneo la Mizani Ndolela mkoani Iringa leo, ikiwa ni michezo wa kombe la Mei Mosi inayoendelea mkoani hapa. Mshindi alitumia dakika 32:18. (Picha Zote na Bahati Mollel wa TAA).


Na Bahati Mollel-TAA, Iringa
TIMU ya Uchukuzi imetwaa ubingwa wa mchezo wa baiskeli wa kilometa 20 kwa wanawake na wanaume baada ya wachezaji wake Chaptele Muhumba na Scolastica Hasiri kuibuka washindi, katika michuano ya Kombe la Mei Mosi inayoendelea mkoani Iringa.

Mbio hizo zilizoanzia eneo la mizani Ndolela na kuishia FFU, ambapo Muhumba alimaliza baada ya kutumia muda wa dakika 32:18; huku Scolastica akimaliza kwa dakika 53:44.
Wachezaji na viongozi wa michezo mbalimbali ya timu ya Uchukuzi wakiwa katika picha ya pamoja na mshindi kwa upande wa wanaume, Chaptele Muhumba (aliyevaa kofia nyeusi katikati), baada ya kuibuka mshindi kwa kutumia dakika 32:18 katika michuano ya kombe la Mei Mosi inayoendelea mkoani Iringa.
Ushindi wa pili kwa wanaume ulichukuliwa na Nehemia Jonnas wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) aliyemaliza kwa muda wa dakika 41:44 na mshindi wa tatu ni Stanley Umbe wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa dakika 46:51. Aliyeshika nafasi ya nne ni Roman Steven wa MUHAS aliyetumia saa 1:12.40 na wa mwisho ni John Fataki wa Ikulu.

Kwa upande wa wanawake mshindi wa pili Happy Mwanga wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) alitumia muda wa saa 1:23.33 na wa tatu ni Severina Mnyaga wa MUHAS alitumia muda wa saa 1:38.00.
Bingwa Bingwa wa wanawake wa mbio za baiskeli, Scolastica Hasiri (mwenye kofia ngumu) akiwa na viongozi na wachezaji wa michezo mbalimbali wa timu yake ya Uchukuzi baada ya kuibuka mshindi katika michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika leo kwa kushindanishwa kilometa 20. Scolastica alitumia muda wa dakika 53:44.


Katika mchezo wa netiboli, timu ya Ikulu iliwaadhibu Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa kuwafunga magoli 70-4 katika mchezo uliofanyika leo  kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki (RUCU).

Washindi walikwenda mapumziko wakiwa mbele kwa magoli 33-2. Mfungaji Fatuma Machenga wa Ikulu ndio aliyefunga magoli yote 70, huku kwa upande wa Tanesco yamefungwa na Imelda Hango.

  1. Mlinzi Jacky Sanga (WD) wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) akijitahidi kuzuia mpira uliorushwa na Fatuma Fusi (WA) wa Ikulu katika mchezo wa netiboli wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika leo kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki (RUCU) mkoani Iringa. Ikulu wameshinda kwa magoli 70-4. 

Katika mchezo wa soka nao ulifanyika leo kwenye uwanja wa Samora, mabingwa watetezi timu ya Geita Gold Mine (GGM) wameendelea kugawana pointi na wapinzani wao ambapo wamelazimishwa sare na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya bao 1-1.

GGM ndio walikuwa wa kwanza kupachika bao katika dakika ya 27 lililofungwa na Mohamed Salum, lakini TRA wakasawazisha kwa njia ya penalti kupitia kwa Boniface Emmanuel katika dakika ya 52.
Mfungaji Mfungaji Caltace Manampo (GA) wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) akidaka mpira uliorushwa na Pendo Rungu (WA-njano) huku Restituta Karani (WD) na Lilian Sylidion (GD) wote wa Ikulu wakijaribu kutibua harakati za mfungaji huyo katika mchezo swa netiboli wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika leo kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki Iringa (RUCU). 


Wakati huohuo, michuano hiyo ya Mei Mosi yenye kaulimbiu “Tanzania ya Viwanda Swadakta… kwa Ukuzaji wa Ajira Sambamba na Uhamasishaji wa Michezo Kazini”, inafunguliwa rasmi kesho tarehe  23 April, 2018 na Mkuu wa Mkoa wa Iringa,  Amina Masenza, ambapo zaidi ya timu 12 zinashiriki katika michezo ya netiboli, soka, karata, bao, draft, baiskeli na riadha.
Winga Winga Pendo Rungu (aliye  na mpira) wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) akitafuta njia ya kupasia mpira mfungaji wake Imelda Hengo (GS-njano) huku Chuki George (mwenye ribbon ya njano kichwani) wa Ikulu akijaribu kukwapua mpira huo katika mchezo wa netiboli wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika leo kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki (RUCU).  



No comments:

Post a Comment