Sunday 29 April 2018

Simba Yainyoosha Yanga Uwanja wa Taifa


Na Mwandishi Wetu
VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba wamezidi kuukaribia ubingwa baada ya leo kuibuka na pointi zote tatu kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Yanga katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

Bao hilo pekee lililoifanya Simba kuzidi kuukaribia ubingwa ambao kwa mara ya mwisho waliutwaa katika msimu wa mwaka 2011-12, lilifungwa na Erasto Nyoni katika dakika ya 37 kwa kichwa akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Shiza Kichuya na kuparazwa na Rafael Daud na kumkuta mfungaji.

Yanga walijikuta wakicheza pungufu baada ya mchezaji wake Hassan Kessy kutolewa baada ya kupewa kadi ya pili ya njano kutokana na kumchezea vibaya Asante Kwasi katika dakika ya 48.

Pamoja na kucheza pungufu, lakini Simba walishindwa kutumia nafasi hiyo kupata bao jingine na badala yake kila dakika zilipotokomea, waliendelea kucheza kwa kujihami zaidi na kurudi nyuma.

Hatahivyo, Simba ndio walitawala zaidi mchezo huo, ambapo walipata jumla ya kona nane wakati watani zao Yanga hawakupata kona yoyote huku Yanga wakiwa nakadi mbili za njano wakati Simba moja na washindi walipiga mashuti matano yaliyolenga bao wakati Yanga mawili tu.

Kwa ushindi huo, Simba imefikisha pointi 62 na sasa kuhitaji pointi sita tu ili kujihakikishia ubingwa kwani Yanga akishinda mechi zake zote sita zilizobaki atafikisha pointi 66 tu, ambazo zitakuwa zimepitwa na Wekundu wa Msimbazi.

Baada ya kipigo hicho, Yanga wanaendelea kuwa katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi zao 48 wakiwa pointi moja nyuma ya Azam FC, ambayo iko katika nafasi ya pili licha ya kucheza mechi 26 wakati Yanga wamecheza jumla ya mechi 24.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Nyoni ambaye alifunga bao hilo pekee alisema kuwa wao wamepania kila mechi kupata pointi tatu na alifanikiwa kufunga bao hilo baada ya mabeki wa Yanga kuwabana wafungaji wa Simba, Emmanuel Okwi, Shiza Kichuya na John Bocco.

Endapo Simba itatwaa ubingwa wa Tanzania Bara, itapata nafasi ya kuliwakilisha taifa katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika msimu ujao.

Kikosi Simba kilikuwa: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Nicholas Gyan/ Paul Bukaba, Yusufu Mlipili, James Kotei, Jonasi Mkude, Asante Kwasi, Shomari Kapombe, John Bocco, Emmanuel Okwi na Shiza Kichuya.

Yanga:Youthe Rostand, Hassan Kessy, Gadiel Michael, Andrew Vincent, Kelvin Yondani, Said Makapu, Yusuph Mhilu, Papy Tshishimbi/Emmanuel Martin, Obrey Chirwa, Raphael Daud/ Juma Mahadhi  na Ibrahim Ajibu/ Pius Buswita.

                            MP     W       D        L        GF      GA      +/-    Pts    
 Simba                                      26      18       8        0       59      13       46      62     
 Azam                                        26      13       10      3        25      12       13       49     
 Yanga                                      24      13       9        2        40      14       27      48     
 Prisons                                25      9        11        5        22      18       4        38     
 Singida                                 26      9        11        6        23      24      -1       38     
 Mtibwa                                    25      8        9        8        20      19       1         33     
 Lipuli                                       26      7        11        8        19       20      -1       32     
 Ruvu                                        26      8        8        10      26      33      -7      32     
 Stand                                         26      7        8        11        19       30     -11      29     
 Mbeya City                         26      5        13       8        23      30     -7      28     
 Kagera Sugar              26      5        12       9        17       25      -8      27     
 Mwadui                          25      5        11        9        27      34      -7      26     
 Mbao                              25      5        9        11        23      33      -10     24     
 Majimaji                               26      4        11        11        26      36      -10     23     
 Ndanda                          26      4        11        11        17       28      -11      23     
 Njombe Mji                          26      4        10      12       16       33      -17     22


No comments:

Post a Comment