Tuesday 17 April 2018

Wachezaji Mei Mosi 2018 Wasisitiziwa Nidhamu




 Baadhi ya wachezaji wa timu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakisikiliza kwa makini maelekezo mbalimbali yanayotolewa na viongozi wa kamati ya michuano ya Kombe la Mei Mosi katika kikao kilichofanyika jana kwenye uwanja wa Samora, yakiwa ni maandalizi ya michuano hiyo iliyoanza jana (Picha Zote na Bahati Mollel-TAA)

Na Bahati Mollel-TAA, Iringa

WACHEZAJI wanaoshiriki kwenye michuano ya Kombe la Mei Mosi inayoendelea kwenye Uwanja wa Samora mkoani Iringa, wametakiwa kuwa na nidhamu ndani na nje ya uwanja, imeelezwa.

Mjumbe wa Kamati ya michezo hiyo, Bi. Joyce Benjamin amesisitiza wachezaji wote kuzingatia maadili ya utumishi wa umma kwa kuwa na nidhamu popote wanapokuwa kwenye mkoa wa Iringa, ikiwemo ya kuvaa mavazi ya staa na kuwa na kauli nzuri kwa  wachezaji wenzao, viongozi na waamuzi.

Bi. Bebnjamin amesema haipendezi na haileti sifa nzuri kwa wachezaji hao ambao timu zao zinatoka kwenye wizara na taasisi za umma kuonesha utovu wa nidhamu, ambapo watakuwa wamekwenda kinyume na maadili ya utumishi wa umma.

Ofisa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Iringa, Bw. Mweri Kilimali (aliyesimama) jana akielezea kifungu namba 28 kinachohusiana na ubadhirifu wa mali za serikali kwa wachezaji wanaoshiriki mashindano ya Kombe la Mei Mosi yanayofanyika katika uwanja wa Samora. 

“Haitapendeza kumuona mtumishi wa umma ambaye yupo hapa katika michezo amevaa nguo zisizokuwa na staa, fupi, za kuonesha maungo na za kubana na kuja nazo huku uwanjani au kutembea mitaani, pia kutoa kauli chafu kwa wachezaji au viongozi wa timu yake au pinzani au kwa waamuzi, hatutasita kumuandikia barua kali ya karipio na nakala kupelekwa kwa mwajiri wake ili amchukulie hatua zaidi za kinidhamu,” amesema Bi. Benjamin.

Nayo taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa nchini (TAKUKURU), imesema itafanya ukaguzi wa wachezaji wanaoshiriki kwenye michuano hiyo, ili kubaini wachezaji wasio waajiriwa wa serikali ‘mamluki’, kwa kuwa sio sheria kutumiwa kwa wachezaji hao.


Ofisa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Iringa, Bw. Mweri Kilimali (aliyesimama) jana akielezea kifungu namba 28 kinachohusiana na ubadhirifu wa mali za serikali kwa wachezaji wanaoshiriki mashindano ya Kombe la Mei Mosi yanayofanyika katika uwanja wa Samora. 
Akizungumza jana na wachezaji waliowasili mkoani Iringa kwa ajili ya kushiriki kwenye michezo hiyo, Afisa kutoka Takukuru, Bw. Mweri Kilimali amesema endapo watabaini kuwepo kwa wachezaji hao watawachukulia sheria ikiwemo ya kufunguliwa kesi ya uhujumu uchumi na kuingizia serikali hasara.

“Hawa wachezaji wanakuwa wakitumia rasilimali za serikali kwani wanakuwa wamelipiwa posho kutoka serikalini kutokana na taasisi au wizara iliyomsajili, hivyo wote waliohusika akiwemo Afisa Utumishi watachukuliwa sheria kutokana na kuihujumu serikali na watafungwa kutokana na kosa hilo, kwani wanakuwa wamekula njama ya kumsajili mtu ambaye sio mtumishi wa umma na kumlipa posho kutoka katika fungu la fedha za serikali,” amesema Bw. Kilimali.

Wachezaji wa timu ya Uchukuzi wakisikiliza maelekezo yaliyokuwa yakitolewa na viongozi wa Kamati ya Michuano ya Kombe la Mei Mosi katika kikao kilichofanyika jana kwenye uwanja wa Samora, mkoani Iringa. Michuano hiyo itazinduliwa rasmi Aprili 21, 2018 na Mkuu wa Mkoa Mhe. Amina Masenza.  

Bw. Kilimali amewataka viongozi wote wa michezo walioambana na timu zao kuhakikisha wanawasomea wachezaji kanuni hizo za mashindano na kuweka msisitizo kila wakati ili wasiende kinyume na kanukni hizo, hivyo wasidhubutu kufanya kosa la kukiuka na kutumia madaraka yao vibaya na kusajili wachezaji wasiokuwa waajiriwa halali wa serikali, kwa kuwa ni kosa lililopo chini ya kifungu namba 28 cha makosa ya ubadhirifu na watafunguliwa kesi ya uhujumu uchumi kwa kuwa watakuwa wameiingizia serikali hasara.

Naye Katibu Mkuu wa Kamati ya michezo ya Mei Mosi, Bw. Award Safari amesema adhabu mbalimbali zitatolewa kwa watakaochezesha mamluki kwa mujibu wa kanuni za michezo hiyo namba 13.0 kipengele 13.1 ambapo kiongozi au viongozi watakaohusika kumsajili mamluki atafungiwa kwa kipindi cha miaka miwili, huku mchezaji husika ataondolewa katika kituo cha mashindano, na timu husika itapigwa faini ya sh. 500,000.

Bw. Award amesema adhabu nyingine ni timu husika iliyochezesha mamluki itanyang’anywa ushindi endapo itakuwa imeshinda, huku viongozi au kiongozi aliyehusika kusajili mamluki ataandikiwa barua na nakala yake itapelekwa kwa mwajiri wake, ikionesha udanganyifu aliofanya na kuiingizia ofisi yake hasara.

“Ili kudhibiti mamluki lazima kila mwanamichezo atatakiwa kuwa na kitambulisho chake halisi cha kazi, kadi ya bima ya afya, kadi ya mfuko wa jamii  na hati ya malipo ya mshahara yaani salary slips za miezi miwili ya Februari na Machi 2018, na vitatumika kama vielelezo endapo mchezaji yeyote atalalamikiwa kuwa ni mamluki,” amesema Award.

Award amezitaja kanuni nyingine kuwa ni pamoja na usajili ni lazima wachezaji wote wajaze fomu maalumu zitakazotolewa na Kamati ya mashindano itakayokuwa na kmajina na picha yake halali; pia kanuni ya ushindi utatambulika kwa pointi, magoli ya kufunga na kufungwa, na tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa, na endapo timu zitafungana kwa kila kitu basi utaratibu wa kurushwa shilingi utatumika.


No comments:

Post a Comment