Wednesday 18 April 2018

Ikulu Yaiadhibu RAS Iringa kwa Kuwachapa 49-8


Mchezaji  Sharifa Hamis (kulia) akifanya mazoezi ya kucheza bao na Ambakisye Mwasunga (kushoto) wakifanya mazoezi ya kujiandaa na michuano ya Mei Mosi kwa upande wa michezo ya jadi inayofanyika kwenye uwanja wa Somora mkoani Iringa. Katikati ni mchezaji wa mchezo wa draft Bw. Omar Said akiangalia. (Picha na Bahati Mollel-TAA)

 Na Bahati Mollel-TAA, Iringa
TIMU ya Ofisi ya Rais Ikulu imewachapa bila huruma wenyeji RAS Iringa kwa kuwafunga magoli 49-8 katika mchezo wa netiboli wa michuano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki (RUCO) mkoani Iringa.

Ikulu inayofundishwa na kocha mzoefu Mary Protas ambapo wafungaji wake Fatuma Machenga aliibeba timu yake kwa kufunga magoli 48 huku Irene Elias alifunga bao moja pekee. Magoli ya RAS Iringa yamefungwa na Warda Sapal na Zitaamanzia Kididi kila mmoja manne. 

Katika mchezo wa soka timu ya RAS Iringa ilifungwa na Tumbaku ya Morogoro kwa magoli 3-0 katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja w Samora.


 Mshambuliaji Ramadhani Shegodo wa timu ya Tumbaku ya Morogoro, akipiga mpira ulioandikia bao la kwanza dhidi ya RAS Iringa, katika mchezo wa Mei Mosi uliofanyika jana kwenye uwanja wa Samora. Tumbaku wameshinda mabao 3-0.

Washindi walipata bao lao la kwanza kupitia kwa Ramadhani Shegodo aliyefunga dakika ya tisa baada ya kupata pasi kutoka kwa Mohamed Mtawal; huku bao la pili lilipatikana dakika ya 29 kwa shuti  kali la Ushindi Nzogela.

Bao la tatu lilifungwa na Salum Idd katika dakika 52 baada ya kupiga krosi murua iliyomshinda kipa Mashaka Peter aliyejikuta akiusindikiza mpira langoni mwake.

Hatahivyo, Tumbaku itabidi wajilaumu kwa kukosa magoli mengi ya wazi, ikiwemo dakika ya 20 mshambuliaji wake Issa Simbaliana kukosa penalti  iliyotolewa na mwamuzi Steven Makuka baada ya Nzogele kuchezewa rafu na Dickson Kiboye wa RAS Iringa, lakini kwa kupaisha mpira juu ya goli,

 Mfungaji Fatuma Machenga (GS) wa Ikulu akifunga mbele ya mlinzi wa RAS Iringa (GK), Maria Mwita katika mchezo wa netiboli wa mashindano ya Kombe la Mei Mosi uliofanyika jana kwenye uwanja wa Chuo Kikuu cha Katoliki (RUCO) Iringa. Ikulu wameshinda magoli 49-8.

Timu za mchezo wa netiboli zitacheza kwa mtindo wa ligi kutokana na kuwa tano, ambazo ni Uchukuzi, Ikulu, Hifadhi ya Ngorongoro, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na RAS Iringa, ambapo bingwa atapatikana kwa wingi wa pointi na magoli ya kufunga.

Kwa upande wa soka timu zimegawanywa katika makundi mawili, ambapo kundi ‘A’ linaundwa RAS Iringa, Tumbaku, Tanesco na Hifadhi ya Ngorongoro, huku kundi ‘B’ zipo Geita Gold Mine (GGM), Uchukuzi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAO).

No comments:

Post a Comment