Thursday 26 April 2018

Kocha Hatua Yanga, Aipa Mbinu Kumuua Mnyama


Na Mwandishi Wetu
KOCHA mpya wa Yanga, Mwinyi Zahera (pichani) kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) amewapa mbinu wachezaji wa timu hiyo ili kuwafunga mahasimu wao wa jadi, Simba, katika mchezo utakaofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

Mchezo huu unakuja wiki tatu tangu klabu hiyo ikimbiwe na aliyekuwa kocha wake, Mzambia George Lwandamina aliyerejea kwao ikielezwa kujiunga tena na Zesco United ya huko.

Na baada ya waliokuwa wasaidizi wa Lwandamina kuiongoza timu katika mechi tatu bila ushindi, ikitoa sare mbili zote za Ligi Kuu na zote 1-1 dhidi ya Singida United na Mbeya City katikati ya kipigo cha 1-0 cha Wolaita Dicha nchini Ethiopia katika Kombe la Shirikisho, uongozi umeleta kocha mpya.

Huyo ndiye Zahera ambaye baada ya kufika kambini Morogoro alianza kwa kukutana na makocha waliopo, Mzambia Noel Mwandila na wazawa Nsajigwa Shadrack na kocha wa makipa, Juma Pondamali.

Habari kutoka kwenye kambi hiyo ya Yanga zimesema kwamba Zahera amepata fursa ya kuitazama Yanga inavyocheza katika mechi zake kadhaa zilizopita na kuwatazama pia Simba kabla ya kuingia mazoezini kutoa mbinu zake kusaidia maandalizi ya pambano dhidi ya watani Jumapili.

Zahera hatakaa benchi Jumapili na kimsingi ataanza kazi rasmi kwenye mechi za makundi Kombe la Shirikisho, Yanga ikianzia ugenini dhidi ya USMA Alger Mei 7, mwaka huu mjini Algiers, Algeria.

Simba ambayo inafundishwa na kocha Mfaransa, Pierre Lechantre anayesaidiwa na Mtunisia, Aymen Mohamed Hbibi, Mrundi, Masoud Juma na mzawa Muharami Mohamed ‘Shilton’, inaongoza Ligi Kuu ikiwa na pointi 59 baada ya kucheza mechi 25, wakati Yanga inafuatia kwa nyuma kidogo wakiwa na pointi 48 baada ya kuingia uwanjani mara 23.

Yanga inazidiwa pointi 11 na Simba SC na ina viporo viwili, maana yake ili kutetea ubingwa wao, itabidi washinde Jumapili na washinde mechi zao zote zilizobaki za Ligi Kuu, huku wakiwaombea mahasimu wao hao wapoteze mechi nyingine pia moja, jambo ambalo sio rahisi.

No comments:

Post a Comment