Monday 16 April 2018

Bayi Apokewa Kifalme Akirejea Kutoka Gold Coast

Filbert Bayi mara baada ya kutua kwenye Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) akitokea Gold Coast, Australia, ambako alipewa tuzo ya kutukuka. Kushoto ni mkewe, Anna Bayi.

Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imezitaka kampuni mbalimbali kujitokeza kudhamini riadha badala ya kung’ang’ania soka.

Bayi akiwasili JNIA.
Hayo yameelezwa mjini Kibaha na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Everist Ndikilo  katika hafla ya kumpongeza mwanariadha wazamani wa Tanzania, Filbert Bayi kwa kupata tuzo iliyotukuka iliyotolewa na Shirikisho la Michezo ya Jumuiya ya Madola (CGF).
Bayi alipewa tuzo hiyo wiki iliyopita wakati wa michezo hiyo iliyomalizika juzi Gold Coast, Australia kufuatia mchango wake katika michezo hiyo, ikiwemo kuweka rekodi ya Madola iliyodumu kwa miaka 44 sasa bila kuvunjwa.

Mwanariadha huyo nguli, aliweka rekodi ya dunia sambamba na ile ya Jumuiya ya Madola ya mbio za meta 1500 mwaka 1970 wakati ile ya dunia ilivunjwa baada ya miaka mitano, lakini ya Madola bado anaishikilia hadi leo.

Wanafunzi wa shule yake wakimsubiri kwenye Kiwanja cha Ndege.
Ndikilo alisema kuwa mafanikio ya Bayi yalikuja kutokana na juhudi zake binafsi pamoja na uzalendo kwa nchi yake.

Alisema makampuni yameng’ang’ania kudhamini soka, hivyo aliyaomba kujitokeza kudhamini na riadha ili kuuletea mafanikio mchezo huo, ambao umeiletea sifa kubwa nchi.
Ndikilo alimpongeza Bayi kwa tuzo hiyo na kuwataka wanariadha chipukizi kujituma zaidi katika mchezo huo, kwani juhudi zinalipa kama alivyofanikiwa Bayi na sasa Jumuiya ya Madola imeamua kumuenzi.

Alisema kuwa mkoa wake uko tayari kushirikiana na kusaidia taasisi yoyote, ambayo itakuwa tayari kusaidia kudhamini mchezo wa riadha ili kuhakikisha unakuwa.

Kwenye Kiwanja cha Ndege, Bayi alipigwa na mshituko baada ya kukutana mapokezi makubwa kutoka kwa wadau wa michezo wa mkoa wa Pwani pamoja na wanafunzi na walimu wa shule yake na kupewa shada la maua huku ukiwa na mabango ya kumpongeza.

Bayi aliwasili kutoka Gold Coast na kupokewa katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) na wadau mbalimbali wa michezo kabla ya kuondoka kwa msafara  mzito ulioongozwa na pikipiki ya usalama barabarani na gari la polisi kwenda Mkuza Kibaha, alikoandaliwa sherehe hiyo ya kumpongeza.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Everisy Ndikilo akimpongeza Bayi pamoja na Kamanda wa Polisi (RPC) wa mkoa huo, Jonathan Shana (kulia) 

Awali, Makamu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau alisema kuwa tuzo hiyo imetokana na utendaji bora na jitihada za Bayi katika riadha, hasa kuvunja rekodi hiyo, ambayo sasa itadumu hadi mwaka 2022.

No comments:

Post a Comment