Monday 2 April 2018

Bayi Apewa Tuzo Iliyotukuka Michezo ya Madola

Rais wa Shirikisho la Michezo ya Jumuiya ya Madola (CGF), Louise Martin (kushoto) akimkabidhi mwanariadha wazamani wa Tanzania, Filbert Bayi tuzo iliyotuka katika hafla iliyofanyika katika hoteli ya Sheraton Grand Mirage mjini Gold Coast, Australia.

Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Michezo ya Jumuiya ya Madola (CGF) limempatia tuzo ya Utumishi Uliotukuka gwiji wa riadha wa Tanzania, Filbert Bayi kutokana na mchango wake katika mchezo huo.

Bayi, alitwaa medali ya dhahabu, ambapo mbali na kuvunja rekodi ya dunia ya mbio za meta 1500 katika Michezo ya Jumuiya ya Madola Chrischurch, New Zealand mwaka 1974, aliweka pia rekodi mpya ya Jumuiya ya Madola, ambayo amedumu nayo hadi sasa, ikiwa ni miaka 44.

Kwa upande wa rekodi ya dunia ya mbio hizo, Bayi ambaye ni Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), alidumu nayo kwa takribani miaka mitano, kabla haijavunjwa na  Sebastian Coe, ambaye kwa sasa ni Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Riadha, IAAF.
Tuzo hiyo, Bayi alikabidhiwa na Rais wa CGF, Louise Martin katika hafla iliyofanyika kwenye hoteli ya Sheraton Grand Mirage mjini Gold Coast, Australia wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa shirikisho hilo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CGF, Ben Nichols, Bayi alipewa tuzo hiyo pamoja na viongozi wengine wa mashirikisho ya michezo kutoka nchi mbalimbali duniani.

Bayi aliliambia Habari Leo jana kwa njia ya simu kuwa, pamoja na jambo la kushtua, lakini kwake jambo muhimu na kubwa ni kutambuliwa kwa juhudi zake.
Alisema jambo jema kama hilo daima ni furaha kubwa na linamkubusha mazuri, ambayo ameyafanya wakati wake akiwa mwanariadha wa kitaifa na kimataifa.

“Mafanikio daima hayaji kirahisi, juhudi binafsi, nidhamu kujituma ni muhimu sana na tuzo hiyo ni kwa ajili ya familia yangu, wanamichezo pamoja na mashabiki wangu, “alisema Bayi.

Akitoa rai, Bayi aliwaomba Watanzania kuwa na utamaduni na kutambua wanamichezo walioliletea taifa heshima katika maeneo mbalimbali, ikiwemo katika michezo pamoja na utendaji mzuri wa kazi.
Alisema kuwa hatua hiyo itahamasisha wanamichezo wadogo na watendaji katika vyama na mashirikisho ya michezo.

No comments:

Post a Comment