Tuesday 30 January 2018

Kiwanja cha Ndege Iringa yaifunga CRDB




Kikosi cha Timu ya soka ya Kiwanja cha Ndege cha Iringa kilichopo eneo la Nduli wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya mchezo wao dhidi ya Benki ya CRDB. Wa kwanza kulia ni Meneja wa Kiwanja hicho, Bi. Hanna Kibopile.

Na mwandishi Wetu
Timu ya soka ya Kiwanja cha Ndege cha Iringa kilichopo eneo la Nduli imewafunga CRDB benki kwa magoli 2-0 katika mchezo wa mashindano ya watumishi wa umma na binafsi yanayofanyika kwenye uwanja wa Lugalo.

Mashindano hayo ya kwanza na ya kuvutia yameanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bi.Amina Masenza ili kuwajengea afya na kujenga uhusiano mzuri kati ya umma na binafsi, ambapo magoli ya Kiwanja cha ndege yalifungwa na Mwika Nyangi na Daniel Mtweve.

Timu 23 zinashiriki kwenye mashindano hayo na zimegawanywa katika makundi manne ambapo timu ya Kiwanja cha ndege cha Iringa inaongoza katika kundi lake la C wakijikusanyia pointi sita (6) baada ya kushinda mechi mbili ilizocheza.

Timu nyingine zinazounda kundi C ni pamoja na Benki ya Posta, Iringa DC, Tanesco na IDY DC, wakati kundi ‘A’  linaundwa na RAS, TANROADS, IRUWASA, TRA, Magereza, DIRA timu za kundi ‘B’ ni Veta, Manispaa, Polisi, Kiumaki na Sido na zinazounda kundi ‘D’ ni Zimamoto na vyuo  vya RUCU, Mkwawa, Iringa, na Kleruu.

Hata hivyo bingwa wa mashindano hayo yanayofanyika asubuhi na jioni katika viwanja vya Chuo cha Mkwawa, Kleruu, Lugalo na Kichangani atazawadiwa sh. 350,000, wakati mshindi wa pili atapata 250,000 na watatu sh.200,000 pia kutakua na zawadi nyingine mbalimbali. 

No comments:

Post a Comment