Monday 8 January 2018

Athumani Juma Chama `Jogoo' Afariki Dunia

Na Mwandishi Wetu
BEKI wa zamani wa Yanga, Athumani Juma ‘Chama Jogoo’ (pichani) amefariki dunia jana usiku katika hospitali ya Rufaa Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya ugonjwa wa kiharusi.

Akizungumza jana Hassan Msumari alisema msiba upo nyumbani kwa marehemu Yombo Makangarawe wilaya ya Temeke na  anatarajiwa kuzikwa kesho katika makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.

“Taratibu za mazishi zitaanzia nyumbani kwa marehemu Yombo Makangarawe na ataswaliwa katika msikiti wa Manyema  saa 7:00 mchana na kuzikwa katika makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam,” alisema Msumari. 

Pia Msumari alisema Chama alistaafu soka mwaka 1990 na alianza kusumbuliwa na maradhi mwaka 2014 na kujikuta akishindwa kumudu kufanya shughuli yake hadi umauti ulivyompata akiwa amelazwa hospitali kwa wiki mbili.

Chama ni jina la utani ambalo marehemu alipewa kutokana na beki wa zamani wa Zambia, Dick Chama (marehemu) ambaye alicheza kwa mafanikio timu ya taifa ya kwao kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia 1967 hadi 1976 na klabu za za Mufulira Wanderers, Green Buffaloes na Bancroft Blades.

Chama alipewa jina hilo baada ya kujiunga Yanga  mwaka 1981 akitokea Pamba ya Mwanza na mashabiki ndio waliombatiza Juma jina hilo baada ya beki wao mwingine, Rashid Idd aliyekuwa akiitwa Chama kuhamia Pan Africans.

Pia alikuwa akijulikana kwa jina lingine la utani, Jogoo ambalo alipewa mwaka 1981 kwenye michuano ya CECAFA Challenge nchini Kenya kutokana na mchezaji mmoja wa Harambee Stars, Sammy Onyango ‘Jogoo’ kutokana na namna alivyokuwa anajua kukaba.

Chama alizidi kupata umaarufu Jangwani kutokana na alivyoweza kumdhibiti mshambuliaji Simba, Zamoyoni Mogela ‘Golden Boy’ katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Lgi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu) ambao ulichezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

Katika soka, Chama alitoka katika klabu ya Pamba FC ya Mwanza alikozaliwa na kukulia kabla ya kujiunga na Yanga na wakati huo alicheza na akina Joseph Fungo, Yussuf Ismail Bana, Ahmed Amasha ‘Mathematician’, Isihaka Hassan Chukwu, Juma Mkambi ‘Jenerali’, Hussein Iddi, Charles Boniface Mkwasa, Abeid Mziba, Elisha John, Ali Mchumila, Makumbi Juma ‘Homa ya jiji’, Omar Hussein ‘Keegan’, Juma Kampala na wengineo.


Mungu Aiweke Roho ya Marehemu Mahali Pema Peponi. Amina.

No comments:

Post a Comment