Sunday 7 January 2018

Simba kufa au kupona Kombe la Mapinduzi Zanzibar leo ikicheza na URA ya Uganda

Na Mwandishi Wetu
KIKOSI cha Simba leo kitakuwa na mtihani mgumu wa kuamua ama kucheza nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi au kurudi Dar es Salaam kujiandaa na mechi za Ligi Kuu wakati itakapocheza na URA ya Uganda katika mchezo wa mwisho wa makundi.

Simba yenye pointi nne katika nafasi ya tatu, inalazimika kushinda mchezo wa leo ili kufikisha pointi saba, ambazo tayari URA wanazo lakini wastani mzuri wa idadi ya mabao ya kufunga unawabeba vinara hao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Katika kundi hilo mabingwa watetezi Azam FC, tayari wameshafuzu kwa kufikisha pointi tisa baada ya kuifunga Simba bao 1-0 juzi, hivyo inasubiri mmoja wapo kati ya URA au Simba kuungana nayo katika hatua hiyo.

Mchezo huo wa leo ambao umepangwa kuanza saa 10: 30 jioni, unatarajiwa kuwa na ushindani mkali, kwani URA siyo timu ya kubeza kwenye michuano hii ilishawahi kutwaa kombe hilo miaka miwili iliyopita kwa kuwafunga Simba kwenye mchezo wa fainali.

URA ndiyo timu pekee ambayo imewafunga mabinghwa watetezui Azam FC katika hatua ya makundi na wanaingia kwenye mchezo huo wakihitaji sare tu ili kupata pointi moja, ambayo itawafikisha pointi nane, ambazo haziwezi kufikiwa na Simba.

Kocha wa Simba Mrundi Masoud Djuma alisema kuwa anatambua kibarua walichokuwa nacho katika mchezo huo, lakini ameahidi kutumia mbinu mbadala tofauti na walizotumia kwenye mechi tatu zilizopita ili kupata ushindi utakaowapeleka nusu fainali.

“Nimchezo mgumu ambao unatulazimisha tucheze kwa kujitolea zaidi ili kupata matokeo, tumejipanga kufanya hivyo kwasababu tunajua matokeo kinyume na ushindi tutakuwa tumeaga mashindano, “alisema Djuma.

Kocha huyo alisema amewaona wapinzani wao katika mechi mbili walizocheza dhidi ya Mwenge na Azam ni timu ambayo inafungika hasa kama watacheza mpira wa kasi na kuwashambulia mfululizo bila kuchoka.

Katika mfumo huo wachezaji Shiza Kichuya na Nicholaus Gyan watalazimika kufanya kazi kubwa ya kukimbia na kupiga krosi kwenye eneo la hatari ili kuwatengenezea nafasi washambuliaji wa kati John Bocco na Moses Kitandu.

Kwaupande wake Kocha Mkuu wa URA, Nkata Paul alisema maandalizi yao kuelekea mchezo huo yamekamilika na wanachosubiri ni kuonesha kile walichodhamiria kukifanya katika mashindano hayo.

Nkata alisema ameiona Simba ni timu nzuri na wanacheza kwa nidhamu kubwa hasa kwenye eneo lao la ulinzi, lakini atahakikisha anakipanga vyema kikosi chake ili kupata ushindi kama walivyo fanya kwa Azam Alhamisi iliyopita.

Safu ya ulinzi ya Simba ambayo inalindwa na mabeki wa tatu kutokana na mfumo wa 3-5-2 inabidi kuwa imara kuwachunga washambuliaji wa URA hasa Moses Sseruyide, Ssempa Charles, Kagaba Nicholas na Bokota Labama, ambao wameonesha makali mechi zilizopita.


Baada ya mchezo huo majira ya saa 2:15 usiku, Yanga watashuka dimbani kucheza na Singida United katika mchezo wa Kundi B zikimilisha hatua ya makundi baada ya zote kufuzu kwa nusu fainali.

No comments:

Post a Comment