Wednesday 17 January 2018

Okwi kuiongoza Simba Kuikabili Singida, Aomba Radhi Benchi la Ufundi na Viongozi kwa Utoro

Na Mwandishi Wetu
WAKATI Simba ikishuka dimbani leo kucheza na Singida United, mshambuliaji wake, Emmanuel Okwi ameomba radhi wachezaji wenzake, viongozi na benchi la ufundi baada ya kukosekana kwenye kikosi hicho kwa muda mrefu bila sababu za msingi.

Akizungumza jana Kocha wa Simba, Masoud Djuma alisema amemsamehe Emmanuel Okwi, kwani aliomba radhi kwake, kwa uongozi na wachezaji wenzake na juzi alianza rasmi mazoezi na timu.

“Unajua binadamu hakuna aliyekamilika cha lazima ni muunganiko wa pamoja, tukianza kunyoosheana vidole nguvu inapungua cha lazima ni kurudisha nidhamu kwenye timu. Hakuna mchezaji au mtu yeyote ambaye yuko juu ya timu, hata rais wa timu hayuko juu ya timu, timu inakuja kwanza halafu mtu baadaye,” alisema Masoud.

Pia Masoud amemuombea radhi Emanuel Okwi kwa mashabiki, akiwataka kuungana ili timu ifanye vizuri katika mchezo wa leo dhidi ya Singida United na michezo ijayo.

Simba ambayo ilikuwa imeweka kambi mkoani Morogoro,  ilirejea Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wa leo dhidi Singida United utakaochezwa kwenye wa Taifa.

Mchezo huo unachezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam baada ya serikali kuruhusu kutumika kwa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara na zile za kimataifa zilizo chini ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF).


Okwi amekuwa na tabia ya kuchelewa kurudi kundini mara anaporuhusiwa kwenda kwao Uganda kutatua matatizo ya kifamilia au anapoitwa katika timu yao ya taifa, The Cranes, ambapo amekuwa akilalamikia na uongozi pamoja na benchi la ufundi kwa kuvuruga ratiba ya mazoezi.

No comments:

Post a Comment