Saturday 13 January 2018

Simba Sports yaiendea Singida United Morogoro

Na Mwandishi Wetu, Morogoro
TIMU ya Simba imewasili mjini Morogoro kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo wake ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Singida United utakaofanyika Januari 18, kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Simba imeweka kambi katika Chuo cha Biblia, Bigwa mjini Morogoro na jana jioni ilitazamiwa kuanza mazoezi kabambe kujiandaa na mchezo huo unaotarajiwa kuwa wa ushindani mkali kutokana na timu zote kuwa kwenye mbio za ubingwa.

Mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi aliyekuwa kwao kwa sababu ya mapumziko maalum aliyopewa kupata ahueni ya maumivu yake amepona na inaelezwa kuwa amesharejea.

Kipa namba moja, Aishi Manula aliyepewa ruhusa ya kwenda kufunga ndoa, kipa namba mbili Said Nduda aliyekuwa majeruhi, wote wako kambini Morogoro.

Na baada ya timu kufanya vibaya kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi Visiwani Zanzibar, viongozi wanatarajiwa kukutana na wachezaji ili kuwarudishia morali iliyopotea kabla ya mchezo na Singida.

Simba inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 26, sawa na Azam FC, wakiizidi kwa pointi tatu Singida United na tano mabingwa watetezi, Yanga SC.

Ligi Kuu iliendelea jana baada ya mapumziko ya wiki mbili kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambayo ilifikia kilele usiku na Azam FC kutwaa taji baada ya kuifunga kwa penalti 4-3 URA ya Uganda kwenye Uwanja wa Amaan.

Lipuli jana iliikaribisha Mtibwa Sugar na kupokea kichapo cha bao 1-0 kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa, huku Stand United ikiichapa Ruvu Shooting kwa bao 1-0 kwenye  Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga huku Ndanda wakitoa sare ya kufungana bao 1-1 na Mbao kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.

Jumapili, mahasimu wa Jiji la Mbeya, Tanzania Prisons na Mbeya City zitakutana kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na kesho Janauri 15, Njombe Mji wataikaribisha Kagera Sugar FC Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe na Jumatano, Yanga SC watakuwa wenyeji wa Mwadui FC Uwanja wa Uhuru mjini Dar Es Salaam.


Mzunguko wa 13 utahitimishwa kwa michezo miwili Januri 18, Simba wakiikaribisha Singida United kwenye Uwanja wa Uhuru na Maji Maji wakiwa wenyeji wa Azam FC Uwanja wa Maji Maji mjini Songea.

No comments:

Post a Comment