Monday 8 January 2018

Coutinho Atambulishwa Rasmi Barcelona leo

BARCELONA, Hispania
KIUNGO Mbrazil Philippe Coutinho ametambulishwa rasmi leo katika klabu yake mpya ya Barcelona huku akisema kuwa, kutua Barca ni sawa na “ndoto yake kutimia.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 leo alitua rasmi kwa  vigogo hao wa Hispania kufuatia kukamilika kwa ada ya uhamisho ya pauni milioni 142 baada ya kukubaliana na Liverpool.

Muda mfupi alitumia kupiga picha kwenye Uwanja wa Nou Camp baada ya timu ya Barcelona kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Levante katika mchezo wa La Liga.

Coutinho jana alisaini rasmi mkataba wa miaka mitano kabla hajatambulishwa rasmi.

"Habari zenu mashabiki wa Barca, tayari niko hapa, ndoto yangu imetimia na ninatarajia kuwaona hapa kesho (jana), “alisema katika ujumbe wake wa video kupitia Twitter.

Baadae, katika mahojiano na BarcaTV, Coutinho aliongeza kusema anafurahi kucheza pamoja na wachezaji kama Lionel Messi na Luis Suarez.

"Nimefurahi kuwa pamoja nao, nitaweza kujifunza kutoka kwao na kuweza kushinda mechi pamoja.”

Mchezaji huyo amesaini mkataba wa miaka mitano na nusu wenye thamani ya pauni milioni 355.

Ni moja ya mikataba ghali zaidi kuingiwa katika kipindi chote, ukipitwa tu na ule wa pauni milioni 200 wa Paris St-Germain walipoilipa Barcelona wakimnunua Neymar mwaka jana, na ule wa pauni milioni 165.7 wa Kylian Mbappe ambao utaigharimu PSG atakapomaliza kucheza Monaco kwa mkopo.

Akizungumza baada ya mchezo dhidi ya Levante, kocha wa Barcelona Ernesto Valverde alisema ni “mapema mno” kuamua nafasi ipi Coutinho atacheza katika kikosi chake.

Kumekuwa na fununu za mufa mrefu kuwa mchezaji huyo anaweza kucheza pamoja na Lionel Messi na Luis Suarez katika safu ya ushambuliaji au kuwa mbadala wa kungo Andres Iniesta mwenye umri wa miaka 33.

"Anafunga mabao na kutengeneza mabao pia, na anacheza mbele anaweza kutusaidia sana kwa kuwa anaweza kucheza kote….”


Valverde ana amini kuwa Coutinho anaweza kuimarisha kikosi chake ambacho kipo pointi nane kileleni mwa msimamo wa La Liga.

No comments:

Post a Comment