Friday 2 February 2018

TAA Yaikabidhi Zimamoto JNIA Gari Toyota Hilux

*Pia Yaahidi Kuipatia Sh milioni 120 Kwa Ajili ya Mafunzo
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Richard Mayongela (kushoto) akimkabidhi funguo ya gari , Kamishna Generali wa Idara ya Zimamoto  na Ukoaji nchini, Thobias Andengenye katika hafla iliyofanyika leo kwenye Kiwanja cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imekabidhi gari kwa Idara ya Zimamoto ya Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), ili kuboresha utendaji kazi.

Akikabidhi gari hilo katika hafla fupi iliyofanyika leo katika Idara ya Zimamoto kiwanjani hapo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Richard Mayongela alisema gari hilo litasaidia usafiri kwa mkuu wa idara hiyo kiwanjani hapo Kamishna Msaidizi, Christom Manyologa.
Mayongela alisema kuwa gari hilo aina ya Toyota Hilux lenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 80, mbali na kusaidia usafiri kwa bosi huyo wa Zimamoto, pia litasaidia kwa shughuli zingine.

Alisema Zimamoto ni miongoni mwa wadau wakubwa wa TAA, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha wanawezeshwa kutekeleza shughuli zao bila matatizo yoyote.

Mbali na kutoa gari hilo lenye namba za usajili STL 5570,pia TAA imesema kuwa itaipatia Zimamoto kiasi cha Sh milioni 120 kwa ajili ya kuwapatia mafunzo wafanyakazi wa idara hiyo ya Zimamoto katika viwanja vya ndege.

Bosi huyo wa TAA alisema kuwa, mafunzo kwa Zimamoto ni muhimu sana, kwani wanahitaji kwenda na wakati na kujifunza mambo mapya, kwani wengi wao kwa muda mrefu hawajapata mafunzo yoyote.
Alisema TAA itaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na idara hiyo ya Zimamoto, ambao ni miongoni mwa wadau wakubwa wa viwanja vya mdege.

Naye Thobias Andengenye, ambaye ni Kamishna Generali wa Zimamoto na Ukoaji nchini, baada ya kupokea gari hilo, aliishukuru TAA kwa msaada huo na kusema utasaidia sana.

Alisema viwanja vya ndege ndio lango kuu la kuingilia wawekezaji na watalii, hivyo usalama ni jambo muhimu sana.

Alisema bila usalama wawekezaji hao na watalii wataogopa au kushindwa kuingia nchini kuwekeza na kufanya utalii.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Richard Mayongela akizungumza na waandishi wa habari leo baada ya kukabidhi gari kwa Idara ya Zimamoto ya Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA)
Hafla hiyo iliyofanyika katika eneo la idara hiyo katika kiwanja cha JNIA na kuhudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa TAA pamoja na JNIA na wale wa Zimamoto.

Alisema gari alilokuwa akilitumia bosi huyo wa Zimamoto Jnia ni chakavu, hivyo hilo walilopewa litasaidia kufanikisha shughuli mbalimbali.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini, Thobias Andengenye akizungumza na waandishi wa habari leo baada ya kupokea gari lililotolewa na TAA jijini Dar es Salaam.








No comments:

Post a Comment