Saturday 13 January 2018

Azam FC Mabingwa Tena Kombe la Mapinduzi 2018

Na Mwandishi Wetu
AZAM FC imefanikiwa kutetea Kombe la Mapinduzi kwa mara nyingine tena baada ya kuibuka na ushindi wa penalti 4-3 dhidi ya URA ya Uganda kufuatia kumaliza suluhu katika dakika 90 za mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Shujaa wa mchezo huo na mchezaji aliyeibeba Azam hadi kuendelea kulibeba taji hilo ni kipa Mghana, Razack Abalora aliyezuia penalti mbili mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein aliyekuwa mgeni rasmi katika kipute hicho.

Abalora aliye katika msimu wake wa kwanza Azam FC tangu asajiliwe kutoka West African Football Academy (WAFA FC) ya Ghana, alipangu penalti ya kwanza ya URA iliyopigwa na Parrick Mbowa na kuiweka timu yake katika nafasi nzuri ya kutetea ubingwa kabla ya kufanya hivyo tena penalti ya mwisho ya Brian Majwega.

Waliofunga penalti za Azam ni nahodha Himid Mao, Yakubu Mohammed, Enock Atta Agyei na Aggrey Morris wakati Bruce Kangwa alimpelekea mikononi mpira kipa wa URA, Alionzi Nafian na penalti za URA zimefungwa na Charles Ssempa, Shafiq Kagimu na Jimmy Kulaba.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa mkongwe visiwani hapa, Mfaume Nassor aliyesaidiwa na Mbaraka Haule na Dalila Jaffar, dakika 90 zilikuwa ngumu timu zote zikishambuliana kwa zamu na ziwaendee makipa wa timu zote, Abalora na Alionzi Nafian kwa kuokoa vizuri.

Ushindi huu unamaanisha Azam FC wanatwaa Kombe la Mapinduzi kwa mara ya nne ya rekodi, baada ya awali kulibeba pia katika miaka ya 2012, 2013 na 2017 wakiipiku Simba SC ya Dar es Salaam iliyotwaa mara tatu 2008, 2011 na 2015.    

Yanga  ndiye bingwa wa kwanza wa Kombe la Mapinduzi mwaka 2007 wakati timu nyingine zilizotwaa taji hilo ni Miembeni mwaka 2009, Mtibwa Sugar mwaka 2010 na KCCA ya Uganda mwaka 2014.

Jumla ya timu 11 zilishiriki michuano ya mwaka huu, ambazo ni URA, Jamhuri, Mwenge, Azam na Simba zilizokuwa Kundi A na Zimamoto, Mlandege, Yanga, JKU, Taifa Jan’gombe na Singida United zilizokuwa Kundi B.

Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Razack Abalora, Himid Mao, Bruce Kangwa, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, Abdallah Kheri/Joseph Mahundi (dk59), Stephan Kingue, Frank Domayo/Iddi Kipagwile (dk58), Salmin Hoza, Bernard Arthur/Shaaban Iddi (dk58) na Yahya Zayed/Enock Atta-Agyei (dk64).


URA;Alionzi Nafian, Enock Kibumba, Brian Majwega, Allan Munaaba, Patrick Mbowa, Julius Mutyaba, Nicholas Kagaba, Kalama Deboss/Charles Ssempa (dk66), Moses Sseruyide/Peter Lwasa (dk81), Hudu Mulikyi na Shafiq Kagimu/Jimmy Kulaba (dk82).

No comments:

Post a Comment