Monday 1 January 2018

DStv Kuingia Mkataba Mnono na RT

Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Multchoice-Tanzania Januari 4 inatarajia kuingia mkataba mnono na Riadha Tanzania (RT) kwa ajili ya kuisaidia timu ya taifa ya mchezo huo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana, RT na Multchoice- Tanzania kupitia king’amuzi chake cha DStv watakutana jijini Dar es Salaam na kusaini mkataba wa miaka mitatu wa mamilioni ya fedha.

Whlhelm Gidabuday
Katibu Mkuu wa RT, Wilhelm Gidabuday alikiri jana kwa njia ya simu kutoka Arusha kuwa, Januari 4 watakutana na DStv na kuingia mkataba mnono kwa ajili ya kuisaidia timu hiyo ya taifa ya mchezo huo.

Pamoja na kutokuwa wazi ni kiasi gani cha fedha kitakachotolewa na DStv, Gidabuday alisema ni mkataba mnono, ambao utaiwezesha timu yao kujiandaa vizuri kwa mashindano mbalimbali.

Alisema mbali na kambi ya Michezo ya Jumuiya ya Madola, mkataba huo utasaidia pia maandalizi ya timu yao kwa ajili ya mashindano ya dunia ya riadha mwaka 2019 na Michezo ya Olimpiki 2020 Tokyo, Japan.

Alisema mkataba huo utasaidia kuiwezesha Tanzania kupata medali ya dhahabu katika mashindano ya dunia ya riadha pamoja na Olimpiki, medali ambazo bado hatujawahi kuzipata.

“Mkataba huo utatusaidia kuwaandaa wanariadha wetu kutuletea medali za kwanza za dhahabu kutoka katika mashindano ya dunia na Michezo ya Olimpiki, ambayo hatujawahi kuzipata, “alisema Gida.

Alisema kuwa mkataba huo wa miaka mitatu utakuwa ni wa thamani kubwa, ambapo taarifa zingine zilidokeza kuwa ni wa zaidi ya sh milioni 700.

Gidabuday aliendelea kusisitiza kuwa RT wanauwezo wa kuleta medali ya dhahabu kutoka katika Michezo ya Jumuiya ya Madola bila ya kuwepo kwa nyota wa Tanzania, Alphonce Simbu.

Hivi karibuni Gidabuday alikaririwa na gazeti hili akisisitiza kuwa, mwanariadha huyo hatakwenda Gold Coast, Australia katika Michezo ya Madola, kwani anahitaji mapumziko baada ya kushiriki mashindano mengi.

Alphonce Simbu
Hatahivyo, licha ya kusema anahitaji mapuziko, lakini inadaiwa kuwa mwanariadha huyo atashiriki London Marathon, mbio ambazo zitafanyika Aprili mwaka huu sambamba na Michezo ya Jumuiya ya Madola.

Awali, kambi ya timu ya taifa ya riadha kwa ajili ya Michezo ya Jumuiya ya Madola, ilipangwa kuanza Novemba mwaka jana Lushoto, Tanga lakini hadi sasa bado haijaanza ikisubiri fedha hizo.

Taarifa zingine zinasema kuwa kambi hiyo sasa haitakuwa Lushoto na badala yake huenda ikapigwa West Kilimanjaro, ambako ilikaa timu ya taifa iliyoshiriki Olimpiki ya Rio na kumfanya Simbu kumaliza watano.


Simbu Januari mwaka jana alimaliza wa kwanza katika Mumbai Marathon kabla ya kuibuka na medali ya shaba katika mashindano ya dunia ya riadha London, Uingereza Agosti mwaka jana.

No comments:

Post a Comment