Saturday, 24 February 2018

Riadha Tanzania Waitilia Ngumu BMT Tozo Mpya


Na Mwandishi Wetu, Arusha
RIADHA Tanzania (RT) limesema kuwa halitasita tozo za ada mpya za mbio za marathon licha ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuzisitisha hadi watakapokutana Machi 5 mjini Moshi.
RT katika taarifa yake iliyotoa jana imesema kuwa imefedheheshwa na kusitishwa kwa matumizi ya ada mpya kwa waandaaji wa mbio za marathon, ambapo imesisitiza kuwa uamuzi wake uliotolewa Septemba 16 mwaka jana, unabaki pale pale.
 Taarifa iliyotolewa jana mjini hapa na Katibu Mkuu Wilhelm Gidabuday inasema kuwa BMT haiwezi kuipangia RT ada kama ambavyo haiwezi kulipangia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ada za  viingilio kwani RT ni chombo huru.
Alisema kuwa hiyo njia ya RT kujitafutia vyanzo vya mapato ili kutoitegemea serikali katika upatikanaji wa fedha.
“Tunasisitiza kuwa waandaaji wote kuhakikisha wanalipa ada  kulingana  na makundi  yaliyopangwa  na kujisajili  kabla ya kuendesha matukio yao,”anasema Gidabuday.
Anasema kuwa waandaaji wote wanatakiwa kulipa ada zao kwa wakati na wapewea hadi Februari 28 wawe wamekamilisha malipo hayo kabla hawajachukuliwa hatua kali.
Alieleza kuwa kuhusu uamuzi wa BMT kuitaka RT kukutana pamoja na waandaaji wa mbio ni jambo ambalo halitawezekana kutokana  na  kuwa Kamati ya Utendaji haitaweza kuhudhuria kikao hicho kilichoitishwa Machi 5 mjini Moshi.
 “Sababu ya  kushindwa kuhudhuria ni kutokana  na wito mfupi wa kikao hicho, ambapo wajumbe wengi watakuwa wametawanyika sehemu mbalimbali kutokana na majukumu  ya chama, ikiwemo kushughulikia  kambi ya taifa,”aliongeza.
 Gidabuday alifafanua kuwa BMT mara nyingi iliwahi kuihimiza RT ikae na waandaaji ili kupunguza msururu wa mbio  za marathon ambazo hazina tija kwa taifa.
“Ikumbukwe  kuwa Chama cha Waandaaji wa Mbio sio mdau wa RT kwa maana hakitambuliki  rasmi kwetu,wadau halali wa RT ni waandaaji wa mbio ambao wamejisajili na kulipa ada,”alisema.
 Aliisihi BMT kushughulikia masuala ya kiufundi na uhuru wa kikatiba  wa vyama vya michezo ili kuepusha migongano ambayo itarudisha nyuma maendeleo ya michezo.

No comments:

Post a Comment