Sunday 11 February 2018

Simba Yahamishia Makali ya Ligi Kuu Kimataifa


Na Mwandishi Wetu
SIMBA imeendekeza makali yake ya katika Ligi Kuu hadi katika mashindano ya kimataifa baada ya kuichalaza Gendarmerie mabao 4-0 katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la Afrika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.


Wawakilishi hao kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho walianza kuhesabu mabao dakika ya kwanza ya mchezo huo baada ya Said Ndemla kufunga kwa mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja kutikisa nyavu.

Nahodha wa Simba, John Bocco alifunga mabao mawili katika mechi hiyo, dakika ya 32 alilolifunga baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Gendarmerie na dakika ya 45 alipofunga bao la kichwa akiunganisha krosi ya Emmanuel Okwi.

Simba ilitawala katika kila idara kwenye kipindi cha kwanza, lakini hali ilibadilika kwenye kipindi cha pili baada ya wapinzani wao kuonekana kujizatiti zaidi.

Pengine baada ya kujiuliza na kujirekebisha, dakika ya 90, Okwi aliandika bao la nne kwa Simba kwa mpira wa adhabu ulioanzishwa na Erasto Nyoni kabla ya ‘Mhenga’ huyo kuuwahi na kuujaza wavuni.

Shujaa mwingine katika mechi ya jana alikuwa kipa wa Simba, Aishi Manula aliyeoangua penalti katika dakika ya 50.

Penalti hiyo iliyopigwa na Abdorahim Mohammed ilitolewa na mwamuzi baada ya James Kotei wa Simba kumchezea rafu Ahamed Aden wa Gendarmerie.

Matokeo hayo yanaiweka Simba nafasi nzuri ya kusonga mbele kwani sasa wapinzani wake watalazimika kushinda 5-0 katika mechi ya marudiano ili wasonge mbele.

Akizungumza baada ya mechi hiyo, nahodha wa Simba, John Bocco alisema wamefurahia matokeo hayo na sasa wanaiandaa na mechi za Ligi Kuu kwani lengo lao ni kufanya vizuri.

Simba endapo itavuka raundi hii, raundi inayofuata huenda ikakabiliana na kibarua kigumu kutoka ama timu ya Misri au kwingineko kwenye soka kubwa zaidi.

No comments:

Post a Comment