Tuesday 27 February 2018

KAMATI YA MAADILI YAWAFUNGIA VIONGOZI MVUVUMWA KWA KUGHUSHI LESENI ZA WACHEZAJI


Na Mwandishi Wetu

KAMATI ya Maadili ya TFF iliyokutana Februari 3, 2018 na Februari 17, 2018, katika ofisi za TFF Karume, pamoja na mambo mengine yaliyojadiliwa pia ilipitia na kutoa hukumu ya tuhuma za kutoa taarifa zisizo sahihi na kughushi leseni za usajili zilizowakabili watuhumiwa mbalimbali walioletwa mbele yake.

Tuhuma hizo zilitokana na mechi namba 26 Kundi A ligi daraja la kwanza iliyofanyika Oktoba 29, 2017 kati ya Mvuvumwa FC na Friends Rangers ambapo katika mchezo huo timu ya Mvuvumwa FC iliwachezesha wachezaji watano (5) ambao ni Elias Costa Elias (jezi namba 5), Lukwesa Joseph Kanakamfumu (jezi namba 7), Dunia Abdallah Dunia (jezi namba 1), Doto Justine Kana (jezi namba 12) na Mwarami Abdala Mwarami (jezi namba 8).

Kamati imemtia hatiani kocha na mratibu wa Mvuvumwa FC, Joseph Kanakamfumu kwa makosa yote mawili, kutoa taarifa zisizo sahihi, (udanganyifu) ili kufanikisha usajili wa wachezaji kinyume na taratibu za ligi daraja la kwanza.

Kosa la kwanza Kanakamfumu akiwa kocha wa Mvuvumwa FC aliwaorodhesha wachezaji (Elias Costa Elias, Lukwesa Joseph Kanakamfumu, Dunia Abdallah Dunia, Doto Justine Kana Mwarami Abdala Mwaram) kushiriki mechi namba 26 huku akijua kwamba hawana leseni halali kutoka TFF, wachezaji wote walitoka katika kituo ‘academy’ anayoiendesha hivyo ni dhahiri alijua alichokuwa anakifanya.

Kosa la pili Kanakamfumu aliamua kuwaongeza wachezaji hao baada ya kukabidhiwa timu kwa vile alifahamu uwezo wao na inaonekana alitumia uzoefu wake katika mpira wa miguu kupata leseni za kughushi.

Kwa makosa hayo, kamati inamfungia Joseph Kanakamfumu kutojihusisha na shughuli za mpira wa miguu kwa kipindi cha miaka mitano.


No comments:

Post a Comment