Monday 12 February 2018

JNIA kuingizia TAA Sh milioni 253 kwa mwaka

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Makame Mbarawa (kulia) akipokea taarifa ya mchakato wa vyanzo vya mapato katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), leo katika Jengo la kufikia na kuondokea abiria mashuhuri (VIP) Terminal Two kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Profesa Ninatubu Lema.

Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) itaongeza pato lake kwa kiasi cha Sh milioni 253 kwa mwaka kutokana na ungezeko la tozo la pango la ardhi watakalotozwa wapangaji katika Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.

Hayo yameelezwa leo na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TAA, Mhandisi Profesa Ninatubu Lema wakati akisoma taarifa ya wataalam kuhusu mchakato wa vyanzo vya mapato katika  Kiwanja cha JNIA kwa Waziri wa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Makame Mbarawa.
Mhandisi Profesa Ninatubu Lema akisoma taarifa yake leo mbele ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Makame Mbarawa. 
Profesa Lema alisema kuwa ongezeko hilo la fedha ni sawa na asilimia 35 mara baada ya kuanza kwa utekelezaji wa yalioyoridhiwa katika majadiliano ya mikataba husika.

Alisema kuwa mikataba karibu yote ya TAA imetoa mwanya wa kurejea tozo ya ardhi nay a tahafifi (review of land lease and concession rates) kila baada ya miaka miwili, zoezi la majadiliano na watoa huduma litakuwa endelevu na litakapofanyika litahusisha wataalam kutoka taasisi nyingione, pale panapohitajika, kama ilivyofanyika mwaka huu.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Makame Mbarawa (kulia) akizungumza leo. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Richard Mayongela.
Taarifa hiyo ilihusu majadiliano yaliyofanyika na watoa huduma/wafanyabiashara katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere yamevaa matunda baada ya baadhi ya maeneo kukubalika, ambayo ni pamoja na ongezeko la tozo ya pango la ardhi (toka dola za Marekani 5.00 hadi 7.90) na riba ya ucheleweshaji malipo ambayo ni asilimia moja.

Profesa aliongeza kusema kuwa timu hiyo ya wataalam pia ilipendekeza tozo ya tahafifu kuwa kati ya asilimia 15 ya mapato ghafi kwa mwaka.
Mbarawa aliipongeza timu hiyo ya wataalam kwa kazi waliyofanya, lakini alisisitiza kuwa wapangaji wa kiwanja hicho wasinyanyashwe na wale watakaozembea kulipa pango wasionewe huruma.

Alisema ni aibu kwa taasisi yenye uwezo wa kujiendesha kwa kutumia vyanzo vyake, kupiga hodi serikali na kuomba omba fedha kila siku.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Richard Mayongela akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha kukabidhi taarifa ya wataalamu kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Makame Mbarawa (kushoto)..
Wakati huohuo, Serikali imesema  mchakato wa uboreshaji wa Shirika la ndege la Tanzania(ATCL) unaoendana  na ununuzi wa ndege mpya unaoendelea kufanywa na Serikali hivi sasa, umelenga kuliboresha shirika hilo kwa lengo la kulikuza kibiashara ndani na nje ya Tanzania na hivyo kuliingizia fedha na hivyo kukuza uchumi wa taifa.

Profesa Mbarawa aliyasema hayo leo baada ya kutembelea ujenzi wa sehemu ya tatu ya jengo la abiria la JNIA (Terminal 3) unaotekelezwa na Kampuni ya Ujenzi ya Bam International ya Uholanzi, ambao umekamilika kwa takeibani asilimia 68.5 na unatarajia kukamilika Septemba mwaka huu.

No comments:

Post a Comment