Monday 12 February 2018

Zuma Apewa Saa 48 Kuachia Ngazi Urais

Rais Jacob Zuma

JOHANNESBURG, Afrika Kusini
RAIS wa Afrika Kusini Jacob Zuma amepewa saa 48 kujiuzulu mara moja nafasi yake hiyo ya uongozi, imeelezwa.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari likiwemo Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini (SABC), hatua hiyo imekuja baada ya mazungumzo ya zaidi ya saa 10 yaliyofanywa na chama tawala cha African National Congress (ANC) katika mkutano wa dharura mapema leo Jumatatu.

Vyanzo hivyo vya habari vinasema kuwa, kikao hicho kiliwaagiza watu wawili akiwemo Rais wa sasa wa ANC, Cyril Ramaphosa kwenda kumuona uso kwa uso Zuma na kumueleza maamuzi ya kikao hicho ya kumtaka kuachia ngazi ndani ya saa 48.

Inaelezwa kuwa Zuma ametakiwa kujiuzulu la sivyo chama hichi kitamtoa madarakani mara moja.

Hatua hii ya ANC inaonekana ndio njia rahisi zaidi ya chama hicho kumshinikiza rais Zuma kuondoka madarakani badala ya kusubiri utaratibu wa Bunge ambao ungeweza kuwa mrefu na wenye madhara zaidi kwa ANC.
Rais wa ANC, Cyril Ramaphosa

Rais Jacob Zuma ambaye anakabiliwa na mashtaka kadhaa ya rushwa, alishindwa uongozi wa chama tawala Desemba mwaka jana.

Rais mpya wa ANC, Ramaphosa ndiye anayeongoza shinikizo za kumuondoa Zuma katika nafasi yake hiyo ya Urais, na hatimaye kushika nafasi hiyo.

Ramaphosa ameahidi pia kupambana na rushwa iliyokithiri na kukijenga upya chama, wakati nchi hiyo ikielekea katika Uchaguzi Mkuu mwakani.

No comments:

Post a Comment