Friday 25 August 2017

Kiwanja cha JNIA Terminal 3 kufungwa mitambo ya kisasa kubaini waliomeza dawa za kulevya

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Salim Msangi akizungumza na Kamati ya  Kamati ya Ardhi na Mawasiliano ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar waliotembekea mradi wa ujenzi wa Terminal 3 jijini Dar es Salaam leo.

Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege (TAA) imesema itafunga mitambo ya kubaini watu waliomeza dawa za kulevya katika jengo la abiria namba tatu (Terminal III) kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Hatua hiyo ni katika kupambana na tatizo la dawa za kulevya na kuhakikisha hakuna dawa zinazopitishwa kupitia uwanja huo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Salim Msangi (kushoto) akielezea jambo wakati wa ziara ya wajumbe wa Kamati ya Ardhi na Mawasiliano ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar 
 Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Salim Msangi wakati akijibu maswali mbalimbali ya wajumbe wa Kamati ya Ardhi na Mawasiliano ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar waliotembekea mradi wa ujenzi wa jengo hilo leo.

Msangi alisema, mbali na mtambo huo kufungwa katika kiwanja huo ili kuhakikisha hakuna dawa zinazopitishwa lakini pia taasisi nyingine mbalimbali ikiwemo za madini zitakuwa na nafasi katika uwanja huo ili kuhakikisha hakuna madini yanayotoroshwa kwenda nje ya nchi.

"Ni jengo la aina yake kwa kweli, kwa sababu tunataka Airport ya Dar es Salaam iwe ni kiunganishi cha kwenda sehemu nyingine lakini pia kwa kuwa tunafufua shirika letu la ndege iwe ni sehemu ambapo safari zinaanzia hapa na kwenda kuchukua watu katika nchi mbalimbali na kuwaleta hapa," alisema.
Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar wakitembelea Kiwanja cha Kimataifa cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA) Terminal 3 leo jijini Dar es Salaam

Msangi alisema, hatua hiyo itasaidia kuongeza fedha za kigeni na mapato kwani ndege zilizonunuliwa na serikali zitaweza kwenda katika nchi mbalimbali na hivyo kuleta watalii nchini.
Aidha, alisema sambamba na mradi huo pia wana mpango wa kujenga hoteli ya kisasa karibu na uwanja huo ili kuwarahisishia abiria na wageni ambao wanapenda kukaa karibu na uwanja wa ndege.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Zanzibar, Mohamed Ahmed Salim alisema, kupitia ziara hiyo wamejifunza mambo mengi ambayo wataenda kuangalia namna ya kuyaweka katika mradi wa ujenzi wa jengo la abiria namba mbili (Terminal II) katika Uwanja wa Ndege wa Zanzibar.
Alisema mradi huo awali ulikwama kutokana na changamoto mbalimbali lakini kwa sasa wameshafikia muafaka na kwamba ujenzi utaanza muda wowote kuanzia sasa na utachukua miezi 18.

"Kwa mwaka jana uwanja ule umehudumia wageni miliomni moja, tulikuwa tunalenga kujenga jengo litakalohudumia abiria milioni moja nukta mbili lakini kwa kuangalia idadi ya watalii inavyoongeza na dira ya maendeleo tukasema ni bora jengo la kuhudumia abiria milioni moja nukta sita," alisema Salum.
Alisema hatua hiyo ilisababisha kuchelewa kuanza kwa ujenzi kwa kuwa walikuwa kwenye majadiliano ya wafadhili wa mradi huo ambao ni China kupitia Benki ya Exim China.

Naye Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hamza Hassan Juma alipongeza maendeleo ya ujenzi huo pia kupongeza hatua ya serikali kujenga awamu ya pili kwa kutumia fedha za ndani.


"Hii ni nzuri sana, kwasababu inaonesha kuna mambo tunaweza sisi wenyewe, bila kutegemea misaada. Pia tumejifunza mengi tukirudi Zanzibar tutaishauri serikali," alisema Juma.
 


No comments:

Post a Comment