Friday 25 August 2017

Pazia Ligi Kuu msimu wa 2017/18 kufunguliwa kesho

Kikosi cha Simba
Na Mwandishi Wetu
MABINGWA wa Ngao ya Jamii na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) au Kombe la FA Simba ya Dar es Salaam ni miongoni mwa timu 14 zitakazoshuka dimbani kesho kuanza mchakamcahaka wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Simba leo itakuwa mwenyeji wa Ruvu Shooting ya mkoani Pwani katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Wekundu hao wa Msimbazi wameanza msimu huu vizuri kwa kutwaa Ngao ya Jamii Jumatano kwa kuwafunga watani zao wa jadi Yanga kwa penalti 5-4.

Timu hiyo ina usongo wa kufanya vizuri msimu huu baada ya kushindwa kutamba kwa karibu misiimu minne na hivyo kushindwa kushiriki michuano ya kimataifa.

Mbali na mchezo huo, pia kutakuwepo mechi zingine za Ndanda FC kukutana na Azam FC katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona huku Mwadui ikiwa mwenyeji wa Singida United.

Singida imepanda daraja na imefanya usajili wa nguvu na hivyo kuwa moja ya timu ambazo zinapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri msimu huu.

Kagera Sugar ya Bukoba itawakaribisha wagumu Mbao FC katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba huku Mtibwa Sugar ikiikaribisha Stand United kwenye Uwanja wa Manungu Turiani, timu iliyopanda daraja ya Njombe Mji itacheza na Tanzania Prisons na Mbeya City itakwaana na Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine.

Ligi hiyo itaendelea tena keshokutwa kwa mchezo mmoja wakati mabingwa watetezi Yanga watakaikaribisha timu iliyopanda daraja ya Lipuli ya Iringa katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru.

Timu za Njombe Mji, Lipuli na Sigida United zinashiriki ligi baada ya kupanda daraja kuchukua nafasi ya zile zilizoshushwa daraja za African Lyon, JKT Ruvu na Toto Africans, ambazo zitashiriki Ligi Daraja la Kwanza.

Makocha mbali mbali wa klabu ya Ligi Kuu wametambiana, ambapo kocha mkuu wa Mwadui FC Jumanne Ntambi amesema timu yake ipo tayari kwaajili ya mchezo dhidi ya Singida united wikiendi hii katika Uwanja wa Mwadui Complex.


Akielezea kuhusu maandalizi ya mchezo huo,Kocha huyo wa zamani wa timu za Panone,JKT Mlale na Kahama United alisema katika michezo michezo yao ya kirafiki waliocheza mpaka sasa wameweza kugundua makosa yao.

No comments:

Post a Comment