Tuesday 29 August 2017

Samatta atua kuiongezea nguvu Taifa Stars

Na Mwandishi Wetu
MCHEZAJI wa kimataifa wa Tanzania anayecheza soka nchini Ubelgiji, Mbwana Samatta amewasili katika kokosi cha timu ya taifa, Taifa Stars, kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Botswana.

Timu hiyo imeanza mazoezi kwenye Uwanja wa Uhuru au Shamba la Bibi jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kipute hicho, ambacho kipo katika ratiba ya mechi za kirafiki za Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA).

 Samatta anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji pia ndiye nahodha wa Taifa Stars.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas amesema kuwa, wachezaji wote wanaocheza hapa nchini waliingia kambini jana, huku wanaocheza nje wakitarajiwa kuwasili kuanzia leo.

“Jana jioni wachezaji wa timu za Azam FC, Yanga pamoja na Simba SC waliingia kambini na kikubwa cha kwanza Daktari wa timu aliwapima afya zao leo asubuhi na jioni timu ikaanza mazoezi Uwanja wa Uhuru, “amesema.

Lucas amesema kwamba msafara wa wachezaji 18 na viongozi tisa kutoka Botswana unatarajiwa kuwasili Alhamisi kabla ya kufanya mazoezi katika Uwanja utakaotumika kwa mechi Ijumaa.
“Wenzetu tumewasiliana nao na wamesema watakuja na wachezaji 18 na viongozi tisa, 

tunazungumzia msafara wa watu 27 na timu itafika Agosti 31, lakini hatujajua ni muda gani watawasili,”amesema.

Lucas amesema wamekwishafanya mawasiliano na wachezaji wanaocheza nje walioitwa kujiunga na kikosi cha Stars akiwemo Nahodha,  Farid Mussa wa CD Tenerife  ya Hispania, Simon Msuva wa Difaa Hassan El –Jadida ya Morocco na Abdi Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini na wote wanatarajiwa kuanza kuwasili kesho.

Kuhusu suala la Uwanja utakaotumika katika mechi hiyo Alfredy amesema, wamethibitisha Uwanja wa Taifa upo katika ukarabati ulioanza siku tano zilizopita na mchezo dhidi ya Botswana sasa ni rasmi utapingwa Uwanja wa Uhuru.

No comments:

Post a Comment