Tuesday 1 August 2017

RC Mghwira kushiriki Kili FM Marathon 2017

Na Mwandishi Wetu
MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira (pichani), atakuwa mgeni rasmi katika mbio za pili za kimataifa za Kilifm Marathon zitakazofanyika Agosti 13, imeelezwa.

Mghwira hivi karibuni aliteuliwa na Rais Dk John Magufuli kuwa mkuu wa mkoa huo akichukua nafasi ya mtangulizi wake, Said Meck Sadick aliyeomba kujiuzulu.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Moshi mkoani Kilimanjaro mratibu wa mbio hizo, Nelson Mrashani alisema kuwa mkuu huyo wa mkoa amethibitisha kushiriki katika mbio hizo.

Alisema kuwa mbio hizo mwaka huu zinatarajiwa kuwa za aina yake na kushirikisha wakimbiaji kibao kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Mbali na mbio za nusu marathon ambazo ni za kilometa 21, pia kutakuwa na mbio za kilometa tano na zile za watoto za kilometa 2.5 pamoja na zile za walemavu wa ngozi.

Mshindi wa kwanza wa mbio hizo ataondoka na sh 700,000 wakati mshindi wa pili atabeba sh 500,000 huku mshindi watatu atatwaa sh 300,000 na wanne sh 200,000.


Mrashani alisema kuwa mwaka huu wanatarajia kushiriki zaidi ya wanariadha 1,000.

Mwaka 2015, alikuwa mwanamke pekee aliyewania kiti cha Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT), ambapo Magufuli wa CCM, aliibuka mshindi wa kiti hicho.

No comments:

Post a Comment