Saturday, 4 April 2015

Yanga yachapwa Zimbabwe, yasonga mbele CAF
Na Mwandishi Wetu
PAMOJA na kupokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa wenyeji wao wa Zimbabwe FC Platinum, Yanga ya Tanzania imefanikiwa kusonga mbele katika hatua inayofuata ya mashindano ya Kombe la Shirikisho la Afrika.

Kikosi hicho cha Yanga kinachonolewa na kocha Mholanzi Hans van der Pluijm kimefanikiwa kutinga raundi ya pili ya michuano ya  Kombe la Shirikisho Afrika(CAF),kwa ushindi wa jumla ya mabao 5-2.

Bao pekee la FC Platinum hilo lilifungwa katika dakika ya 29 na kiungo Walter Musona, aliyeunganisha krosi ya Brian Muzondiwa akiwa ndani ya eneo la hatari la Yanga na kufanya uwanja wa Mandava uliopo Bulawayo kulipuka kwa shangwe za wachimba Almasi wa Zimbabwe.

Pamoja na Platinum kuanza mchezo huo kwa kasi lakini wachezaji wa Yanga walionekana kucheza kwa kujitolea na umakini mkubwa huku wakifanya mashambulizi ya kustukiza.

Mrisho Ngassa alipoteza nafasi ya wazi dakika ya 22 baada ya shuti alilopiga kupanguliwa na kipa wa Platinum Petros Mhari, hiyo ikiwa baada ya kupokea mpira wa kichwa wa Amissi Tambwe aliyekua ameunganisha kona iliyochongwa na Simoni Msuva.

Vijana wakocha Norman Mapeza walikwenda mapumziko wakiwa hawana furaha baada ya lengo lao la kupata mabao angalau matatu kushindikana na kuendelea kubaki katika wakati mgumu kutafuta mabao manne kipindi cha pili.

Kipindi cha Pili Platinm waliendelea kupambana wakijaribu kutengeneza mashambulizi mengi kwenye lango la Yanga,lakini ngome ya Yanga iliyokuwa ikiongozwa na nahodha wake Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Mbuyu Twite ilikuwa imara kuondoa hatari zote langoni mwao.

Yanga ilionekana kuzinduka mwishoni mwa mchezo huo na kupoteza nafasi mbili za wazi ambazo washambuliaji wake Amissi Tambwe na Msuva walizipata katika dakika za 77 na 84.

Hiyo inakuwa ni mara ya pili kwa kocha wa Yanga kushindwa kupata ushindi inapocheza ugenini kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho mwaka huu mara ya kwanza licha ya kuitoa BDF XI ya Botswana, lakini mechi ya marudiano iliyochezwa Lobatse Botswana ilifungwa mabao 2-1 na kufuzu raundi ya kwanza kwa matokeo ya jumla ya 3-2 na sasa imefungwa 1-0 Ugenini kwenye uwanja wa Mavanda Zimbabwe.

Kwa matokeo hayo, Yanga itacheza na mshindi kati ya Benfica de Luanda ya Angala au Etoile du Sahel ya Tunisia.

Yanga:Ally Mustaph,Juma Abduli, Oscar Joshua,Mbuyu Twite, Nadir Haroub, Said Juma/Kelvin Yondan, Salum Telela,Simon Msuva/Danny Mrwanda, Haruna Niyonzima,Amissi Tambwe,Mrisho Ngassa.

No comments:

Post a Comment