Thursday, 16 April 2015

Lowasa mgeni rasmi bonanza la kupinga mauaji ya maalbino Jumapili
Edward Lowasa.
Na Mwandishi Wetu
ALIYEWAHI kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania Edward Lowasa anatarajiwa kuongoza mbio za pole pole au jogging Jumapili kwa ajili ya kupiga vita mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi Dar es Salaam.

Hivi karibuni nchini Tanzania kumeibuka wimbi la kuwaua au kuwakata viungo walemavu wa ngozi kwa madai ya imani za kishirikina.

Msemaji wa Klabu ya Michezo ya Temeke Family ports Club, Maulid Kisoma, alisema wao kama sehemu ya jamii wameguswa na vitendo viovu wanavyofanyiwa watu wenye ulemavu wa ngozi na hivyo wameamua kuandaa bonanza hilo ili kuelimisha jamii kupitia michezo kuhusu ubaya wa vitendo hivyo.

Alisema bonanza hilo litahudhuriwa na zaidi ya klabu 100 za Dar es Salaam huku zikishirikisha zaidi ya watu elfu tano.

Pia watakuwepo wageni wengine waalikwa wakiwemo Wabunge, Mameya wa Manispaa zote tatu za Dar es Salaam (Kinondoni, Ilala na Temeke), pamoja na viongozi wengine wa kiserikali na taasisi za kijamii.

Mbio hizo zijulikanazo kama mbio za pori zitaongozwa na Lowasa ambaye ndio atakuwa mstari wa mbele kuanzia uwanja wa taifa hadi viwanja vya TCC Chang'ombe, ambako kilele hicho kitakapofanyikia.

"Kutakuwa na michezo mingi  siku hiyo kama vile mpira wa miguu, 
netiboli, na mingine ambapo tunaimani watakaohudhuria watafurahi na kupata ujumbe maalum kuhusu kupinga mauaji ya albino," alisema Kisoma.

 Aliongeza kuwa, "tumewashirikisha ndugu zetu maalbino ambao ndio wahusika na waathirika wakubwa wa kadhia hii ili waje kusimulia jinsi gani wanapata changamoto ya kuishi katika jamii ambayo inawashambulia".

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Maalbino Tanzanzania, Erinest Kimaya alisema wao wamefurahi kupewa mwaliko huo na kwamba wanaona kama jamii haijawatenga na inawasaidia kupambana na ukatili huu.

"Sisi tunafurahi sana tunapoona watu wanajitokeza kutusaidia kupambana na ukatili huu tunaofanyiwa na watu wasiokuwa waadilifu, alisema Kimaya.

No comments:

Post a Comment