Thursday, 2 April 2015

Daba waahirisha mashindano ya vijana ya ndondi


Mwenyekiti wa Chama cha Ndondi Mkoa wa Dar es Salaam (Daba), Karoly Godfrey.

Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Ndondi za Ridhaa Mkoa wa Dar es Salaam (Daba) kimeahirisha mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 15/16 na 16/17 yaliyopangwa kuanza Aprili 1, 2015.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Daba Karoly Godfrey, mashindano hayo sasa yatafanyika Aprili 15 hadi 18 sambamba na Mkutano Mkuu.

Mashindano hayo yatajulikana kama Mashindano ya Ubingwa wa Wazi Kanda Huru ya  Dar es Salaam kuanzia tarehe Aprili 15 hadi 18.

Alitaja sababu za kuyasogeza mbele mashindano hayo ni pamoja na Daba kukosa vifaa vya kuchezea kama glovu na vizuia kichwa au head guards.

Sababu nyingine za kusogeza mbele mashindano hayo ni kukosa medali kwa washindi, ambayo ni muhimu kwa watoto.

Aidha, mwenyekiti huyo alisema kuwa, Daba itafanya mkutano wake mkuu wa kawaida Aprili 16 sambamba na mashindano hayo ya wazi ya vijana.

Ajenda za mkutano huo ni pamoja na kuridhia agenda  za mkutano, kupokea taarifa za  mashindano ya 2014 na  kuridhia utekelezaji  wa mkakati wa  Daba 2014/2017.

Nyingine ni kuridhia Daba kuunda Kamati ya  Kudumu ya  Ufundi na mafunzo na Kamati ya Kudumu ya Fedha na Mipango.

No comments:

Post a Comment