Saturday 7 May 2016

Yanga yatanguliza mguu mmoja makundi Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuikandika Esperanca ya Angola 2-0



Na Mwandishi Wetu
WAWAKILISHI pekee wa Tanzania katika mashindano ya kimataifa Yanga (pichani), leo wamejiweka katika mazingira mazuri ya kucheza hatua inayofuata ya Kombe la Shirikisho la Afrika baada ya kuisasambua GD Esperanca ya Angola katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baada ya kushinda mabao 2-0.

Mashujaa wa Yanga katika mchezo huo ni Simon Msuva na Matheo Antony Simon, baada ya kufunga mabao hayo katika kipindi cha pili cha mchezo huo, ambao unaiweka Yanga katika nafasi nzuri zaidi ya kutinga hatua ya makundi.

Kwa ushindi huo, vijanao hao wa Jangwani sasa wanahitaji sare, au ushindi wa aina yoyote na hata kufungwa 1-0 au kufungwa 2-1 ili kutinga wiki ijayo baada ya mchezo huo wa marudiano utakaofanyika Mei 17 Angola.

Mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe akimtoka beki wa Sagrada Esperanca, Antonio Kasule

Katika mchezo huo uliochezeshwa na waamuzi kutoka Ghana, Joseph Lamptey aliyeuwa kati akisadiwa na David Laryea na Malik Salifu walioshika vibendera, Yanga walipoteza nafasi kibao za wazi za kufunga katika kipindi cha kwanza.

Kinara wa mabao katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Amissi  Tambwe ndiye aliyekosa mabao mengi baada ya kupoteza nafasi nyingi za wazi katika kipute hicho cha leo jijini Dar es Salaam.

Hatimaye chipukizi wa Yanga, Msuva na Matheo wakapeleka raha katika mitaa ya Jangwani Twiga baada ya kufunga mabao hayo mawili yaliyowanyamazisha kabisa Waangola.

Msuva alianza dakika ya 72 akimalizia krosi maridadi ya winga Godfrey Mwashiuya aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Malimi Busungu, kabla ya Metheo kufunga la pili dakika ya 90 kwa shuti la mbali. 

Pamoja na ushindi huo, Yanga ilionekana kabisa kuathiriwa na kuwakosa nyota wake wawili Wazimbabwe, kiungo Thabani Kamusoko na mshambuliaji Donald Ngoma ambao walikuwa wanatumikia adhabu za kadi za njano walizopewa mfululizo kwenye mechi dhidi ya Al Ahly mwezi uliopita.

Kikosi cha Yanga kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Salum Telela/Mbuyu Twite dk46, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Malimi Busungu/Godfrey Mwashiuya dk53, Amissi Tambwe na Deus Kaseke/Matheo Anthony dk77.

No comments:

Post a Comment